ZOGO LA HAMO NA JEMUTAI

Je, Hamo alichujwa, alijiuzulu au ni uvumi tu

Hatima ya aliyekuwa mtangazaji haijabainika wazi baada yake kukosekana hewani tangu mwezi wa Aprili

Muhtasari

Huku Wakenya wengi wakiamini kuwa Hamo alichujwa kwa upotovu wa nidhamu, baadhi ya wandani wake wamekanusha madai hayo wengine wakitangaza kuwa alijiuzulu mwenyewe kwa sababu zake binafsi.

Mcheshi Profesa Hamo
Mcheshi Profesa Hamo
Image: Facebook

Hatima ya kazi yake mcheshi tajika Profesa Hamo kwenye kampuni ya Royal Media Services  imezua gumzo mitandaoni.

Hii ni baada ya mtangazaji  kutosikika hewani kwa kipindi cha takriban wiki mbili zilizopita. Hakuna tangazo lolote rasmi lililotolewa na mtangazaji huyo au kampuni ya RMS  kuhusu kilichomtokea Hamo ambaye amekuwa akishirikiana na mwanahabari Jeff Koinange kwenye kipindi ‘Morning Drive’ kwenye redio ya Hot 96 tangu mwaka wa 2018.

Hata hivyo, nduru za kuaminika zinaarifu kuwa mcheshi huyo wa Churchill si mwajiriwa wa RMS tena. Wengi mtandaoni wamehusisha masaibu hayo ya Hamo na mgogoro uliotokea baina yake na mcheshi mwenzake alamaarufu kama ‘Jemutai’

Mcheshi Jemutai kwenye Jukwaa
Mcheshi Jemutai kwenye Jukwaa

Awali Jemutai alimkashifu Hamo kwa kuwa baba mpotevu. Wawili hao wamezaa watoto wawili pamoja nje ya ndoa ila zogo lilivuma Jemutai alipoweka wazi mtandaoni kuwa amekuwa akishughulikia watoto wale peke yake. Alimtaka Hamo kuwajibika zaidi kwenye jukumu la kulea wana wale.

Zogo hilo lilimchochea Hamo kutaka wawili hao kufanya kipimo cha DNA ili kubaini kuwa kweli wana wale wawili ni wake kweli. Matokeo ya kipimo hicho yalitokea mwanzoni wa wiki na kutangazwa naye Jemutai kupitia kurasa zake za mtandao. Hamo hata hivyo amebaki kimya akionekana kutotaka kuzungumzia swala hilo.

Huku Wakenya wengi wakiamini kuwa Hamo alichujwa kwa upotovu wa nidhamu, baadhi ya wandani wake wamekanusha madai hayo wengine wakitangaza kuwa alijiuzulu mwenyewe kwa sababu zake binafsi.

“Pofesa Hamo hakuchujwa RMS” aliyekuwa mtangazaji wa Hot 96 na Radio Jambo aliandika kwenye mtandao wa Twitter.

Kufikia sasa, Hamo hajatoa tangazo lolote kuhusu hatima yake