BURUDANI NA SIASA

Xtian Dela atangaza nia ya kuwa rais

Mwanablogu Xtian Dela ametangaza kuwa atagombea kiti cha ubunge cha Westlands 2022 aende akikaribia kiti cha urais

Muhtasari

•Dela asema kuwa ataanza na kugombea kiti cha ubunge cha Westlands 2022 ndio akaribie cha urais

•Kwa sasa kiti hicho kimekaliwa na Tim Wanyonyi Wetangula ambaye ni kaka yake Seneta  Moses Wetangula.

Xtian Dela
Xtian Dela
Image: HISANI

Aurther Mandela almaarufu kama Xtian Dela ameonyesha nia yake ya kuwa rais wa Kenya siku moja huku akitangaza kuwania kiti cha ubunge cha eneo la Westlands.

Mwanablogu huyo ambaye pia ni mtumbuizaji na mtangazaji amesema kuwa ni wakati wa vijana kutawala ila si kungoja kesho isiyofika.

"Tumechoka kuambiwa kuwa sisi ni viongozi wa kesho, kesho hii itafika lini? Tunataka kuongoza sasa. Tumechoka kuibiwa na kudharauliwa ni kama Kenya sio yetu. Sharti mapinduzi yaonyeshwe kwenye runinga!!" Dela aliandika huku akizindua kampeni yake ya ubunge wa Westlands.

Katika ujumbe mwingine aliouchapisha Dela, alisema kuwa angeanza na ubunge wa Westlands ndivyo akaribie kiti cha uraisi.

"Natabasamu kwani najua sijaangusha kizazi changu nikiwa rais! Kwa sasa tuanze na kiti cha ubunge cha Westlands 2022 tuendelee tukikaribia kiti cha juu zaidi" Dela aliandika.

Dela amewaagiza Wakenya kumchangia aweze kuwania kiti hicho huku akikiri kuwa siasa sio rahisi na ni ghali.

Kwa sasa kiti hicho kimekaliwa na Tim Wanyonyi Wetangula ambaye ni kaka yake Seneta wa Bungoma na kiongozi wa Ford Kenya, Moses Masika Wetangula. Wanyonyi akichaguliwa kwa muhula wa pili mwakani 2017.