ALISEMA NDIO!

Hongera Guardian Angel na Bi Esther Musila

Esther Musila, 51, akubali ombi la ndoa lake Guardian Angel, 30, siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake

Muhtasari

•Guardian Angel alimuomba ndoa Bi Esther Musila siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake

Guardian Angel akiomba ndoa kwake Esther Musila
Guardian Angel akiomba ndoa kwake Esther Musila
Image: Instagram

Mwanamuziki wa nyimbo za injili, Peter Omwaka almaarufu kwa jina la jukwaani kama Guardian angel kwa sasa ni mtu mwenye raha baada ya ombi la ndoa kukubaliwa na mpenzi wake Esther Musila siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake.

Kupitia mtandao wa Instagram, Guardian Angel,30, ametangaza kuwa Bi Musila alikubali ombi lake lililompata kwa mshangao akiadhimisha kufikisha miaka 51.

"NDIYO!! Asante sana mpenzi wangu.. aliondoka nyumbani akijua kuwa tumeenda kutia saini mpango wa biashara kisha ikawa mshangao wa siku ya kuzaliwa na kisha ikawa siku maalum sana maishani mwangu" Angel aliandika chini ya video inayoonyesha jinsi shughuli hiyo ya kufanya ombi la ndoa na kukubaliwa ilienda.

Wanamitandao wengi  ikiwemo wasanii mashuhuri waliwapongeza wawili hao na kuwatakia maisha mema.

Angel na Musila wamekuwa kwenye uhusiano kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa. Kutoka Radio Jambo, tunawatakia wapenzi hao ndoa yenye heri na upendo mwingi.