"Sina ngori yoyote" Kartelo akanusha madai kuwa alizama kwenye uraibu wa mihadarati

Mcheshi huyo ambaye ni baba ya msichana wa mwaka mmoja ameeleza kuwa amekuwa akishughulikia majukumu mengine ya kinyumbani ndio maana hajapatikana mitandaoni

Muhtasari

•Mara ya mwisho Kartelo kuchapisha mitandaoni ilikuwa tarehe 6 mwezi wa Februari.

•Ameeleza kuwa mama yake alimtaka kusaidia kufuga kuku nyumbani na majukumu mengine.

Kartelo na bintiye
Kartelo na bintiye
Image: Instagram

Mcheshi Nickson Chege almaarufu kama Kartelo ametokea kukanusha madai ya baadhi ya mashabiki kuwa amekuwa mraibu wa madawa ya kulevya.

Kwenye mazungumzo na mcheshi mwenzake, Mulamwah aliyemtembelea siku ya Alhamisi, Kartelo amesema kuwa hakuna shida yoyote iliyomkumba.

Hii ni baada ya Wanamitandao wengi kuulizia sana aliko msanii huyo ambaye alikuja kupata umaarufu mkubwa mwaka wa 2019 baada ya video zake za ucheshi kwa lugha ya kipekee ya sheng kuenea na kuvuma sana mitandaoni.

Mi niko poa, hakuna ngori.. sio lazima kuwe na ngori. Kukosa mitandaoni sio kumaanisha kuna shida” Kartelo alimjibu Mulamwah  baada ya kuulizwa mbona hajaonekana mitandaoni kwa muda mrefu kama ilivyokuwa mazoea yake.

Mara ya mwisho Kartelo kuchapisha mitandaoni ilikuwa tarehe 6 mwezi wa Februari. Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakisema kuwa Kartelo alizama kwenye uraibu wa madawa ya kulevya hadi akashindwa kabisa kutumbuiza mashabiki wake tena.

Msanii huyo ambaye ni baba ya msichana wa mwaka mmoja ameeleza kuwa amekuwa akishughulikia majukumu  mengine ya kinyumbani.

Mimi ni baba ya mtu, bwana ya mtu, mwana wa mtu, binamu na mshirika wa mtu” Alieleza Kartelo.

Ameeleza kuwa mama yake alimtaka kusaidia kufuga kuku nyumbani na majukumu mengine.

Kartelo ambaye alikuwa amepata kazi ya uanahabari kwenye stesheni ya MILELE FM alikataa kusimulia yaliyotokea mpaka akaacha kazi hiyo.

Hata hivyo, ameahidi mashabiki wake kuwa atarejea hivi karibuni