USAHURI WA AKOTHEE

"Ikiwa watafuta mume tajiri, nenda oa benki” Akothee ashauri bintiye

Akothee alitumia siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa bintiye Vesha kumshauri kuhusiana na mambo ya kimaisha

Muhtasari

•“Mume wako anafaa kuwa mwenzako, mpenzi wa roho yako na rafiki yako ila sio mashine ya ATM!! Ikiwa watafuta pesa basi kaolewe na benki. Mwanamke anapendeza zaidi ikiwa anaweza jimudu kifedha. Jimudu kifedha kwanza kisha utafute mume ambaye amejimudu pia.

•Mwanamuziki huyo alimtakia mwanawe heri njema ya kuzaliwa na kumsifia huku akisema kuwa yeye ni mfano wa kuigwa.

Akothee na bnti zake Vesha Okello na Rue Baby
Akothee na bnti zake Vesha Okello na Rue Baby
Image: Instagram

Juni 11 ndiyo siku kitinda mimba wa mwanamuziki na mwanabiashara mashuhuri Akothee anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Akothee aliamua kutumia siku hiyo kushauri binti huyo wake kwa jina Vesha Okello kuhusiana na maswala ya maisha.

Kupitia mtandao wake wa Instagram, amepakia picha ya Vesha na chini yake kuandika pointi kumi za ushauri kwa mwanawe huyo.

Kwenye pointi hizo, Akothee ameonekana kumshauri Vesha sanasana kuhusiana na mambo ya ndoa.

“Chukua muda wako kutafuta mume. Usikubali kutulia na mtu asiye na thamana kwa kuharakishwa na jamii. Hakunatarehe ya mwisho ya kuoleka” Akothee alimuandikia mwanawe.

“Mwanaume aliye maishani mwako yafaa awe na thamana ya kuishi naye. Ni aidha mnaishi pamoja ama mnakufa pamoja. Usikubali kudhulumiwa au kukosewa heshima kwenye ndoa” Aliendelea.

“Mume wako anafaa kuwa mwenzako, mpenzi wa roho yako na rafiki yako ila sio mashine ya ATM!! Ikiwa watafuta pesa basi kaolewe na benki. Mwanamke anapendeza zaidi ikiwa anaweza jimudu kifedha. Jimudu kifedha kwanza kisha utafute mume ambaye amejimudu pia.

Pesa haiwezi kunulia raha wala ndoa, ila itafanya maisha yawe rahisi” Akothee aliandika

Mwanamuziki huyo alisema kuwa mwanaume anafaa kuwajibika huku akimwambia mwanawe  asikubali mume anayemuacha alipe bili bila wasiwasi wowote.

Alimsihi pia kuepuka makundi mabaya ya marafiki.  

“Binadamu ni panya, wanauma na kupuliza” alisema

Akothee alishauri vijana kuangazia maisha yao na kuacha maneno ya mtandao.

“Hakuna anayepakia kufeli au udhaifu wake mtandaoni”

Alishauri vijana kuepuka kulinganisha maisha yao na mambo ambayo wanaona mitandaoni.

Mwanamuziki huyo alimtakia mwanawe heri njema ya kuzaliwa na kumsifia huku akisema kuwa yeye ni mfano wa kuigwa.