Eric Omondi afanywa balozi Tanzania

Msanii huyo ambaye anajitambulisha kama 'rais wa wacheshi barani Afrika' alitangaza uteuzi huo siku ya Alhamisi.

Muhtasari

•Meya wa Temeke, Bw. Abdalla Said Mtinika alimteua mcheshi Omondi kutoka Kenya kama balozi siku ya Jumatano na kumkabidhi bendera ya Manispaa hiyo

•Omondi yuko kwenye  ziara nchini ya kikazi nchini Tanzania na anatarajiwa kufanya tamasha kubwa katika uwanja wa Uhuru tarehe 17 Julai.

Eric Omondi na Meya Mtinika
Eric Omondi na Meya Mtinika

Mcheshi tajika, Eric Omondi amepatiwa jukumu la kuwa balozi wa manispaa ya Temeke nchini Tanzania.

Meya wa Temeke, Bw. Abdalla Said Mtinika alimteua mcheshi Omondi kutoka Kenya kama balozi siku ya Jumatano na kumkabidhi bendera ya Manispaa hiyo.

"Nakukabidhi hii bendera Eric Omondi. Uwe balozi wa manispaa ya Temeke. Uitangaze Temeke na sisi tutafanya kazi pamoja.Temeke tuna mambo mengi; waweza wakaja watalii, waweza wakaja wawekezaji,tunahitaji wafanyabiashara. Waambie Temeke ni nyumbani, tangaza Temeke" Bw Mtinika alimwambia Omondi.

Msanii huyo ambaye anajitambulisha kama 'rais wa wacheshi barani Afrika' alitangaza uteuzi huo kupitia mtandao wa Instagram siku ya Alhamisi.

Omondi ameahidi kutekeleza majukumu  yake vyema huku akimshukuru Meya kwa kumkabidhi wadhifa huo.

"Ningependa kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa makubwa anayoendelea kunitendea. Leo nimepewa jukumu kubwa maishani ya kuwa balozi wa Temeke na mkuu wa Temeke Bw.Abdallah Said Mtinika , Mstahiki Meya. Na mimi nitayatekeleza majukumu haya kwa umakini  sana. Nitaipa nguvu yote" Omondi alisema.

Omondi yuko kwenye  ziara nchini ya kikazi nchini Tanzania na anatarajiwa kufanya tamasha kubwa katika uwanja wa Uhuru tarehe 17 Julai.

Ziara ya 'Omondi Stadium Tour' kisha itaelekea kwenye uwanaja wa Jamhuri jijini Dodoma , Uwanja wa Kirumba na kisha uwanja wa Sheikh Abeid Amani Karume mjini Arusha.

"Uwanja wa Uhuru upo hapa kwetu Temeke na tamasha kubwa ya kihistoria na kipekee tutaifanya hapa Uhuru Stadium tarehe 17 Julai. Ningependa kusema asante kwa uongozi wote wa Temeke wakiongozwa na Meya.  Shukrani kubwa pia zimuendee ndugu na baba wa sanaa, Mkubwa Fella kwa kuniung mkono kwenye shughuli hii" Omondi aliandika.