"Mimi ndiye mzuri, nampenda Yesu" Ringtone akashifu Bahati kwa kugura injili

Hapo awali, Ringtone alikuwa amesuta vikali Bahati kufuatia wimbo 'Fikra za Bahati' akisema kuwa alikuwa ameacha injili na kuwa mraibu wa dawa za kulevya

Muhtasari

•Ringtone amepakia video ambayo inaonekana kumkejeli Bahati kwenye mtandao wa Instagram.

•"Hii ndio sababu Wakenya wamechoka na wasanii wa injilil  ila si wote wabaya. Mimi ndiye mzuri hapa, nampenda Yesu" Ringtone aliandika chini ya video ya kukejeli Bahati ambayo alipakia.

Ringtone na Bahati
Ringtone na Bahati
Image: Hisani

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko ameendelea kumkosoa mwanamuziki mwenzake Kevin Bahati kwa kuimba nyimbo ambazo haziambatani na injili.

Ringtone amepakia video ambayo inaonekana kumkejeli Bahati kwenye mtandao wa Instagram.

Video hiyo inaonyesha kumbukumbu ya hafla ya kutuza wasanii wa injili ya Groove Awards mwaka wa  2015 ambapo Bahati alinyakua tuzo  nne . Alishinda tuzo la mwanamuziki bora wa kiume huku wimbo wake 'Barua' ukimshindia tuzo la; video ya mwaka, wimbo wa mwaka na wimbo uliopakuliwa zaidi.

Alipokuwa anapokea tuzo hizo, Bahati aliapa hadharani kuwa hatawahi acha Mungu.

"Naapa mbele ya Dunia, Mungu sitawahi kuacha.  Wajua huu wimbo niliandika wakati watu walikuwa wanasema nalia sana" Bahati anasikika akisema kwenye video hiyo.

Punde baada ya maneno hayo, maneno ya wimbo 'Bahati wachana na sisi' wake DK Kwenye Beat yanayosema ni heri asikie njaa kuliko amsikize Bahati yanachezwa.

Nyimbo zake za hivi karibuni zimeibua utata huku wengi wakiamini kuwa amegura injili. Wimbo 'Fikra za Bahati' ndio ulioibua gumzo kubwa kwani maneno ya Bahati kwenye wimbo huo yalikuwa ya kudhalilisha wasanii wengine huku akionekana akivuta sigara kubwa kwenye video ya wimbo huo.

Ringtone alikuwa amesuta vikali Bahati kufuatia wimbo ule huku akisema kuwa alikuwa ameacha injili na kuwa mraibu wa dawa za kulevya.

 Ameendelea kusema kuwa matendo ya wanamuziki wa injili kuimba nyimbo zenye utata na wengine kugura ndio maana Wakenya wamechoka nao.

"Hii ndio sababu Wakenya wamechoka na wasanii wa injilil  ila si wote wabaya. Mimi ndiye mzuri hapa, nampenda Yesu" Ringtone aliandika chini ya video ya kukejeli Bahati ambayo alipakia.

Willy Paul ni baadhi ya wanamuziki ambao wameweka wazi kuwa wamegura injili.

Siku chache zilizopita, Willy Paul alieleza kuwa ubaguzi, mapendeleo , chuki kutoka kwa wasanii wenzake na wacheza santuri na nyimbo zake  kukosa kuchezwa ndio sababu aliamua kubadilisha sekta ya nyimbo.