Jemutai aandikia Hamo ujumbe maalum kuadhimisha siku ya kina baba

Mwezi uliopita, Hamo aliweka wazi kuwa atamuoa Jemutai kama mke wa pili

Muhtasari

•Jemutai alipakia picha ya Hamo kwenye mtandao wa Facebook akiwa amemshika bintiye na kufuatanisha na ujumbe wake maalum.

•Kwenye kipindi cha maswali na majibu katika mtandao wa Intagram mwezi uliopita, shabiki mmoja alitaka kujua kama Hamo angemuoa Jemutai kama mke wa pili.

Jemutai na Hamo
Jemutai na Hamo
Image: Hisani

Siku ya Jumapili ilikuwa siku ya kusherehekea kina baba duniani na mamilioni ya Wakenya waliitumia kupongeza na kutakia baba zao heri njema.

Wengi walipakia baba zao  kwenye mitandao ya kijamii na kuambatanisha na jumbe maalumu huku  wanawake wakipakia baba za  watoto wao.

Mcheshi Stella Bunei almaarufu kama Jemutai hakuchelewa kumtakia baba ya wanawe wawili ambaye ni mcheshi mwenzake, Profesa Hamo.

Jemutai alipakia picha ya Hamo kwenye mtandao wa Facebook akiwa amemshika bintiye na kufuatanisha na ujumbe wake maalum.

"Siku njema ya kina baba na hongera kwa wimbo wako mpya, msanii amejitolea, Hamo The Profesa" Aliandika Jemutai huku akiwasihi mashabiki wake kutazama wimbo mpya wa Hamo. 

Kwa upande wake Hamo aliandika ujumbe akiwatakia siku njema ya kina baba wote.

"Siku njema ya kina baba kwa baba wote. Kando na wimbo baba Ibrahimu alikuwa na watoto wengi, wimbo upi mwingine mtanipendekezea" Hamo aliandika.

Wawili hao walitumbuiza Wakenya na drama si haba mwezi uliopita baada ya kufichuka wazi kuwa Hamo ndiye baba wa watoto wote wawili wa Jemutai, jambo ambalo lilikuwa fiche kwa muda mrefu.

Drama ilianza wakati Jemutai aliweka wazi kuwa Hamo hakuwa anawajibikia wanawe wawili ambao walikuwa wamepata pamoja.

Madai hayo yalishangaza wengi ambao hawakuwa na taarifa kuwa wawili hao walikuwa wapenzi kwa muda.

Ingawa Hamo alikuwa amekanusha madai hayo na hata kuagiza kufanyiwa kwa vipimo vya DNA ili kudhibitisha watoto ni wake, ilikuja kujulikana wazi kuwa yeye ndiye baba rasmi.

"Matokeo ya DNA yametoka, 99.9%" Jemutai aliandika kwenye mtandao wa Facebook kuthibisha kuwa Hamo ndiye baba.

Tangu hapo, wawili hao wameonekana kuwa katika hali ya maelewano huku Hamo akiapa kuwa atamuoa Jemutai kama mke wa pili wiki tatu zilizopita.

Kwenye kipindi cha maswali na majibu katika mtandao wa Intagram mwezi uliopita, shabiki mmoja alitaka kujua kama Hamo angemuoa Jemutai kama mke wa pili.

"Naam, tumetoka mbali" Hamo alijibu.

Shabiki mwingine alitaka kujua kama wamesuluhisha  ugomvi na 'Baby Mama' wake(mama watoto)

"Yeye sio Baby Mama, ni mke wangu" Hamo alimjibu.

Kwa upande wake Jemutai alikiri kuwa alikuwa amemsamehe Hamo kwa yaliyotendeka.