BET AWARDS 2021

"Wewe bado ni simba" Bahati amfariji Diamond baada ya kukosa tuzo la BET

Bahati amemhimiza Diamond kutia bidii ili kupata mafanikio makubwa zaidi siku za usoni.

Muhtasari

•Bahati amemsifia mwanabongo huyo kwa mafanikio mengi ambayo amekuwa nayo kwenye taaluma ya usani na kumtaja kama shujaa anayewapa watoto wa jamii ya Waswahili msukumo wa maisha.

• Diamond aliibuka wa tatu kwenye tuzo la BET ambalo lilinyakuliwa na mwanamuziki matata kutoka Nigeria, Burna Boy.

Bahati na Diamond
Bahati na Diamond
Image: Instagram

Bahati amemfariji mwanamuziki mwenzake kutoka Tanzania, Diamond Platnumz baada ya kuwa wa tatu kwenye tuzo la BET kitengo cha 'Best International Act'.

Bahati amemsifia mwanabongo huyo kwa mafanikio mengi ambayo amekuwa nayo kwenye taaluma ya usani na kumtaja kama shujaa anayewapa watoto wa jamii ya Waswahili msukumo wa maisha.

Kupitia mtandao wa Instagram, Bahati amemhimiza Diamond kutia bidii ili kupata mafanikio makubwa zaidi siku za usoni.

"Kakangu  mkubwa @DiamondPlatnumz wewe bado ni mshindi. Umepata mafanikio mengi ukiwa na umri mdogo bado na mtu asikudanganye. Umepatia watoto wengi wa jamii la Waswahili msukumo wa maisha na umewafanya kujua kuwa waweza toka kutoka nunge na kuwa shujaa. Umeshinda tuzo la BET tayari kupitia mkono wako mwingine;Rayvanny. Kaka turudi tena kazini na tutazamie makubwa zaidi, Grammys labda. Najivunia uwakilishaji wako wa jamii ya Waswahili. Simba asipo mshika swara hapungukiwi kuwa simba na kuwa fisi. Nakukumbusha kuwa wewe bado ni simba" Bahati alimwandikia Diamond.

Diamond aliibuka wa tatu kwenye tuzo la BET ambalo lilinyakuliwa na mwanamuziki matata kutoka Nigeria, Burna Boy.

 Aya Nakamura wa Ufaransa, alikuwa wa pili kisha Diamond. 

Rayvanny kutoka Tanzania alishinda tuzo la BET kitengo cha 'Best International Viewers' Choice' mnamo mwaka wa 2017.