AFUENI YA HARAKA JAGUAR

Wasanii wajumuika kumtakia Jaguar afueni; Ringtone afanya maombi hospitalini

Mwanamuziki Bahati ambaye alitua nchini kutoka Tanzania jioni ya Jumatatu pia alifika hospitalini kumwona aliyekuwa msanii mwenzake

Muhtasari

•Wakenya ikiwemo wasanii na watu mashuhuri wameendelea kumfariji na kumtakia afueni mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mwanamuziki mashuhuri kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa siasa

•Gabu wa P-Unit alihakikishia Wakenya kuwa Jaguar anaendelea vyema hospitalini na kuwa hayuko katika hali na hatari.

Ringtone akimuombea Jaguar hospitalini
Ringtone akimuombea Jaguar hospitalini
Image: Hisani

Habari za kulazwa hospitali kwa mbunge wa Starehe, Charles Njagua Kanyi, almaarufu kama Jaguar zilienea sana siku ya Jumatatu baada ya kusambazwa kwa video iliyochapishwa na mwanamuziki DK Kwenye Beat.

Kwenye video hiyo, Jaguar alionekana akiwa anasukumwa kwa machela na wahudumu wa afya akiwa katika hospitali moja ambayo haijafichuliwa.

Kulingana na DK Kwenye Beat, Jaguar  huyo alifanyiwa upasuaji wa mguu kufuatia maumivu.

Wakenya ikiwemo wasanii na watu mashuhuri wameendelea kumfariji na kumtakia afueni mwanasiasa huyo ambaye alikuwa mwanamuziki mashuhuri kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa siasa.

DK Kwenye Beat ambaye alifichua kulazwa hospitali kwa Jaguar mtandaoni alikuwa wa kwanza kumfariji rafiki yake kwa ujumbe wa kumpea motisha.

"Wewe ni jasiri na hakuna chochote ambacho kinaweza kuweka chini. Pigana na  wakati na uwe na upone kabisa kwa haraka" DK aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Wanamitandao walifurika chini ya ujumbe wa DK na jumbe za kumfariji Jaguar.

Mwanamuziki mwinigine ambaye alikuwa ameandamana na Jaguar kuenda hospitali ni Gabu wa kikundi cha muziki cha P-Unit.

Gabu alihakikishia Wakenya kuwa Jaguar anaendelea vyema hospitalini na kuwa hayuko katika hali na hatari.

"Mhesh ako sawa. Mungu ni mwema manze" Gabu aliandika.

Mwanamuziki Bahati ambaye alitua nchini kutoka Tanzania jioni ya Jumatatu pia alifika hospitalini kumwona aliyekuwa msanii mwenzake. Bahati alimtakia Jaguar kupona kwa haraka.

"Kutoka uwanja wa ndege moja kwa moja hadi hospitalini . Nilikuja kumtakia Mheshimiwa Jaguar afueni ya haraka na kumuonyesha video yangu mpya" Bahati aliandika.

Mwanamuziki wa nyimbo za injili, Ringtone Apoko pia alifika kumuona Jaguar na akarekodi video akimuombea afueni.  

Ringtone alieleza uhakika wake kuwa Mungu amesikia maombi yake na akawasihi Wakenya kuendelea kumuombea.

Hopekid na mwanamitindo kutoka Tanzania, Jackie Wolper pia walimtakia mbunge huyo afueni.