"Wakenya wakampa nafasi anaweza fanya mapinduzi makubwa" Ali Kiba ampigia debe Joho

Mwanamuziki huyo allisifia sana uzalendo wa Wakenya na akasema kuwa Watanzania wanaiga mfano mwema kutoka kwao.

Muhtasari

•Akizungumza na Jalang'o katika kipindi cha Bonga na Jalas siku ya Alhamisi, Kiba alisema kuwa naibu kinara wa ODM ni mwandani wake.

•Mwanamuziki huyo alimsifia na kumpigia debe sana gavana huyo ambaye ameashiria nia yake ya kuwania urais.

Ali Kiba na Joho
Ali Kiba na Joho
Image: Hisani

Ni dhahiri kuwa mwanamuziki tajika kutoka bongo ana uhusiano wa karibu sana na gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho.

Wawili hao wameonekana hadharani pamoja mara kadhaa huku Kiba akionekana kufanya ziara za mara kwa mara kumtembelea mwanasiasa huyo jijini Mombasa.

Akizungumza na Jalang'o katika kipindi cha Bonga na Jalas siku ya Alhamisi, mwanamuziki huyo alimsifia na kumpigia debe sana gavana huyo ambaye ameashiria nia yake ya kuwania urais.

Alisema kuwa anapendezwa sana na uzalendo wake.

"Wakenya wakampa nafasi anaweza akafanya mapinduzi makubwa sana katika nchi ya Kenya. Yeye  ana maarifa sana na mtazamo wake kwa Wakenya ni mkubwa sana. Wakenya wote ni wazalendo lakini yeye ni mzalendo zaidi

Nimejifunza vitu vingi kutoka kwa Joho kutokana na uzalendo wake sio tu kwa watu wa Mombasa ila kwa Wakenya wote" Ali Kiba alisema.

Mwanamuziki huyo ambaye amekuwa kwenye sanaa ya muziki kwa miaka mingi sana alisema kuwa naibu kinara wa ODM ni mwandani wake.

"Yeye ni  kama ndugu kwangu, ni rafiki yangu mzuri sana" Kiba alisema.

Alisema kuwa wanaheshimiana sana naye licha ya kuwa Joho amemzidia umri na tofauti katika taaluma zao.

"Ananiamini, anaheshimu kichwa changu mimi sio kiasi... Joho anaelewa mimi ni mtu wa aina gani. Mwanzo yeye ni mwanasiasa ambaye namuona ana maarifa mengi sana na Wakenya wakampa nafasi anaweza akafanya mapinduzi makubwa sana." Alisema Kiba.

Alikiba pia alisifia sana uzalendo wa  Wakenya na akasema kuwa Watanzania wanaiga mfano mwema kutoka kwao.

Alisema kuwa Watanzania waliiga mtindo wa kuvaa bangili yenye rangi za bendera ya kataifa kutoka kwa Wakenya.