"Hakuna kinachopiku upendo wa kindugu" Bahati ataja sababu hana ugomvi na Willy Paul na Mr Seed

Mwanamuziki huyo alisema kuwa licha ya tofauti zilizopo, anawaheshimu sana wawili hao haswa akikumbuka walikotoka.

Muhtasari

•Licha ya uwazi uliopo kwamba wasanii hao wana tofauti zao, Bahati ameweka wazi kuwa kamwe hatawahi jibu  au kuzungumza vibaya kuhusu wawili hao.

•Bahati alisimulia tukio moja ambapo Willy Paul, Mr Seed na Jblessings walimtetea asitupwe nje baada yake kuhudhuria hafla ya kuwatuza wasanii bila kualikwa. 

Image: INSTAGRAM//BAHATI

Mwanamuziki maarufu nchini, Bahati ameeleza sababu huwa haenezi ugomvi au kusema vibaya wanamuziki wenzake Willy Paul na Mr Seed.

Licha ya uwazi uliopo kwamba wasanii hao wana tofauti zao, Bahati ameweka wazi kuwa kamwe hatawahi jibu  au kuzungumza vibaya kuhusu wawili hao.

Kupitia ujumbe alioandika kwenye mtandao wa Instagram, Bahati amekiri kuwa Willy Paul na Mr Seed walipata umaarufu mbele yake.

Alisema kuwa alipatana na nyota hao wawili akiwa chini punde baada ya kuondoka katika nyumba ya watoto ya ABC. Kwa wakati huo hakuwa ametambulika, alikiri kuwa Willy na Seed walimsaidia na wametoka mbali.

Bahati alisimulia tukio moja ambapo Willy Paul, Mr Seed na Jblessings walimtetea asitupwe nje baada yake kuhudhuria hafla ya kuwatuza wasanii bila kualikwa. 

"Sikuwa maarufu kwa hivyo sikuwa nimealikwa ila nikapenya ndani na nikaenda hadi kwa kapeti nyekundu ili tu nishuhudie raha iliyoko na nitangaze mgao wangu wa imani nikitumai kuwa siku moja nitakuwa mshindi pia. Shukran kwa Mr Seed, Willy, Jblessing na wengine ambao walinitetea kwa walinzi nisitupwe nje" Bahati alisimulia.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa licha ya tofauti zilizopo, anawaheshimu sana wawili hao haswa akikumbuka walikotoka.

"Hakuna kinachopiku upendo wa undungu na na nathamini hayo" Bahati aliapa.

Bahati ambaye ameendelea kubobea kwenye muziki haswa mwaka huu alisema kuwa huwa anafurahia na  kusherehekea ushindi wa wawili hao.