(+Video) 'Talanta inalipa!' Eric Omondi ajigamba na Sh3M kuonyesha Mutua kuwa yeye sio maskini

Msanii huyo alimkosoa bosi wa KFCB kwa kile alisema ni kukatisha tamaa wasanii wa kizazi kipya na kumshauri kusaidia kugundua na kukuza talanta zao.

Muhtasari

•Baada ya kumkosoa bosi wa KFCB kufuatia matamshi  yake kuwa yeye ni maskini na anapenda kiki, Eric ameamua kupuuzilia mbali matamshi hayo kwa kuonyesha kitita kikubwa cha pesa alichodai kuwa shilingi milioni 3 za Kenya ambazo kulingana naye alipata baada ya kufanya tamasha Tanzania.

Image: INSTAGRAM

Vita kati ya mcheshi tajika Eric Omondi na mkurugenzi mtendaji wa  Bodi ya Filamu na Uainishaji wa Kenya (KFCB) Ezekiel Mutua haina dalili za kuisha hivi karibuni.

Baada ya kumkosoa bosi wa KFCB kufuatia matamshi  yake kuwa yeye ni maskini na anapenda kiki, Eric ameamua kupuuzilia mbali matamshi hayo kwa kuonyesha kitita kikubwa cha pesa alichodai kuwa shilingi milioni 3 za Kenya ambazo kulingana naye alipata baada ya kufanya tamasha Tanzania.

Eric ambaye kwa sasa yumo nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi alijigamba na mabunda ya noti za pesa za Tanzania na kusema kuwa zilikuwa milioni tatu.

"Ezekiel Mutua, hivi ndivyo milioni tatu pesa za Kenya hukaa. Nimeskia umesema kuwa wasanii ni maskini, nimeskia kuwa umesema talanta hailipi, nimeskia umesema wasanii ni ombaomba. Hili ni jasho halali na damu. Talanta halali ambayo Mungu amepeana" Omondi alisema huku akionyesha pesa zile.

Msanii huyo alimkosoa bosi wa KFCB kwa kile alisema ni kukatisha tamaa wasanii wa kizazi kipya na kumshauri kusaidia kugundua na kukuza talanta zao.

"Hautakatisha tamaa wasanii wa wa kizazi kipya. Hautakatisha tamaa ndugu zetu. Talanta inalipa kwa wakati huu.Hili ni tamasha moja tu ambalo nafanya Tanzania. Talanta yalipa na lazima tupatie motisha ndugu zetu wadogo kugundua na kukuza talanta zao"  Omondi alisema.

Hapo awali mcheshi huyo alikuwa amemuita Mutua mwizi na kusema kuwa pesa nyingi alizokuwa amepata ni kutokana na ubadhirifu wa pesa za umma.

Omondi alisema  kuwa pesa zake hutokana na jasho na bidii ambayo anatia kwenye usanii wake.