"Hakuna atakayekuajiri kutokana na huruma!" Akothee awashauri 'single mums' wanaotafuta kazi

Madam Boss amewasihi 'single mums' kutoeleza masaibu yao wanapokuwa kwenye mahojiano ya kutafuta kazi.

Muhtasari

•Mwanamuziki na mfanyabiashara mashuhuri nchini Akothee aliyebandikwa jina  Madam Boss amewasihi kina mama wasimbe (single mums) kutoeleza masaibu yao wanapokuwa kwenye mahojiano ya kutafuta kazi.

•Mama huyo wa watoto watano amewashauri 'single mums' wenzake wasiwahi geuza mahojiano ya kazi kuwa mahakama ya watoto.

Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki na mfanyabiashara mashuhuri nchini Akothee aliyebandikwa jina  Madam Boss amewasihi kina mama wasimbe (single mums) kutoeleza masaibu yao wanapokuwa kwenye mahojiano ya kutafuta kazi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee ambaye huwa anajitambulisha kama 'President of single mothers' amesema kuwa  waajiri huwa hawapatiani kazi kutokana na huruma ama mafadhaiko yaliyokumba mtu.

Mama huyo wa watano na ambaye anaaminika kuwa bilionea amewashauri 'single mums' wenzake wasiwahi kugeuza mahojiano ya kazi kuwa mahakama ya watoto.

"Ukiulizwa suala la mshahara wako, usianze kwa kusema eti 'unajua mimi ni single mother, nahitaji kulipa bili (haya ni mahojiano sio mahakama ya watoto). Hakuna atakayekuajiri kwa sababu ya huruma ama bili zako" Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa kampuni zinalipia thamani ya mtu ila sio wakati wake tu ama hali yake ya  kuwa mama.

"Zuia kutaja masaibu yako kwenye mahojiano na kuharibia mwajiri wako wa awali jina. Ukiulizwa mbona uliacha kazi yako ya awali sema kuwa unataka jukumu mpya na unahisi kwamba mandhari yale mapya yatakupatia nafasi ya kustawi na kuboresha utaalamu wako" Akothee alisema.