Hatimaye kilio cha mwisho cha Omosh kwa Wakenya chaitikwa

"Mimi naweza taka ninunuliwe tu camera, tripod na tulights tuwili na mic sasa niwaache" ndilo lilikuwa ombi la mwisho la Omosh kwa Wakenya.

Muhtasari

•Mwezi uliopita, Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh aliomba kusaidiwa kupata vifaa vya kurekodi michezo yake na kuahidi kuwa hangewasumbua Wakenya tena.

•Ingawa ombi hilo halikupokewa vyema na wanamitandao wengi, mwanamuziki B Classic aliahidi kumtimizia msanii mwenzake ombi lake. 

Image: INSTAGRAM

Hatimaye kilio cha mwisho cha mwagizaji  Omosh kwa Wakenya kimejibiwa.

Mwezi uliopita, Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh aliomba kusaidiwa kupata vifaa vya kurekodi michezo yake na kuahidi kuwa hangewasumbua Wakenya tena.

"Mimi naweza taka ninunuliwe tu camera, tripod na tulights tuwili na mic sasa niwaache" ndilo lilikuwa ombi la mwisho la Omosh.

Ingawa ombi hilo halikupokewa vyema na wanamitandao wengi, mwanamuziki B Classic aliahidi kumtimizia msanii mwenzake ombi lake. 

Kupitia mtandao wa Instagram, B Classic ametangaza kutimiza kwa ahadi yake na akapakia picha akimkabidhi Omosh vifaa vile. 

'Kama nilivyoahidi kuwa nina zawadi ya Omosh ili aweze kupiga kazi na kujiendeleza kimaisha, bai nimefanya sehemu yangu na nimeweza kumpa" B Classic alisema.

Omosh alipokea camera, tripod, kipaza sauti na mataa.

Kwenye tangazo hilo, mwanamuziki huyo pia alidai kuwa Omosh ana kipawa cha kuimba ambacho wengi hawakifahamu bado. Alisema kuwa wanashirikiana kufanya collabo pamoja. 

Wanamitandao wengi wameendelea kumpongeza B Classic kwa kitendo chake cha ukarimu.

Wiki iliyopita Omosh alikabidhiwa nyumba mpya aliyojengewa na baadhi ya wasamaria wema na akaahidi kuwa hataiuza kamwe.