Juma Anderson asimulia alivyotishiwa na mashabiki wa Papa Shirandula kwa 'kumfuta kazi'

Alisema kuwa tukio kama hilo limemfanyikia mara kadhaa.

Muhtasari

•Alipokuwa anazungumza kwenye hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuaga kwa Bukeko, Juma pia alisema kuwa mafanikio yake kwenye sanaa ya uigizaji ni kwa sababu ya Bukeko ambaye aliigiza kama mlinzi wake

•Juma alisimulia jinsi mashabiki wawili wa  Papa Shirandula  ambao alipatana nao alipokuwa anazurura Mumia walimtishia wakitaka kujua mbona akaamua kumpiga kalamu Papa.

Image: HISANI

Mwigizaji William Juma anayefahamika sana kama Juma Anderson kutokana mhusika aliyeigiza kwenye kipindi cha Papa Shirandula amefunguka kuhusu tukio moja ambapo alijipata akikabiliana na mashabiki wa marehemu Charles Bukeko almaarufu kama Papa Shirandula.

Alipokuwa anazungumza kwenye hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuaga kwa Bukeko, Juma pia alisema kuwa mafanikio yake kwenye sanaa ya uigizaji ni kwa sababu ya Bukeko ambaye aliigiza kama mlinzi wake.

Kwenye kipindi hicho, Juma aliigiza kama mwajiri mkali ambaye aliogopwa sana na wafanyakazi wake.

Tukio moja ambapo alimfuta kazi mlinzi wake (Papa Shirandula) lilimletea shida sana akiwa kwenye ziara ya kazi na waigizaji wengine wa kipindi hicho mjini Mumias.

Juma alisimulia jinsi mashabiki wawili wa  Papa Shirandula  ambao alipatana nao alipokuwa anazurura Mumia walimtishia wakitaka kujua mbona akaamua kumpiga kalamu Papa.

"Jamaa wawili waliniona nilipokuwa natembea wakaanza kuulizana,  ''huyu si ni yule mtu ambaye alifuta Papa kazi?' Kama msanii kwa kuwa sikuwa nata kizaaza kutokea, nikaenda pale nikawaambia  kuwa ni mimi ili kukatiza hiyo stori wasije wakaita umati mambo yaharibike" Juma alisema.

Mwigazaji huyo alidhani kuongelesha mashabiki wale kungewatuliza  ila kumbe kwao haikuwa mchezo na walitaka kupata majibu kuhusiana na kitendo cha kikatili ambacho walishuhudia Juma akifanya kwa runinga.

Mmoja wao alimbubujikia matusi akimkashifu kwa ukatili wake hadi Juma aliamua kuondoka  baada ya kugundua kuwa jamaa wale walikuwa na hasira kweli. Alisema kuwa tukio kama hilo limemfanyikia mara kadhaa.

"Mmoja wao alinikemea 'Yaani wewe unakuanga na roho ya shetani namna gani? Uko na roho nyeusi, unaweza aje fukuza aje mtu kwa kazi na  ni mzee atapata kazi ingine wapi. Mtu hata naweza kata mtu na panga, nilidhani ni mchezo kumbe haikuwa mzaha. Niligundua kuwa jamaa hao hawakuwa na mchezo nikaenda. Alikuwa amekasirika sana hata nilihofia maisha yangu kwa wakati mmojaJuma alisimulia.

Siku ya Jumapili, waliokuwa waigizaji wa Papa Shirandula ikiwemo Jalango, Otoyo, Naliaka, Wilbroda, Njoro na wengine pamoja na familia ya Bukeko walifanya hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuaga kwake kutokana na matatizo ya kupumua.