Harmonize aeleza kilichovunja ndoa yake; Amwomba msamaha aliyekuwa mkewe kupitia wimbo

Kwenye wimbo huo, Harmonize amekiri kuwa alikuwa amemficha mtoto huyo wake wa kwanza kwa kipindi cha miezi saba.

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize amekiri kuwa hiyo ndio sababu wakatengana ila akasema kuwa angeonekana mjinga iwapo angeendelea kumficha mtoto wake.

Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Harmonize na mpenzi wake Muitaliano Sarah Michelotti
Image: HISANI

Staa wa Bongo Harmonize ametunga wimbo wa kumuomba msamaha aliyekuwa mpenzi wake Sarah Michelloti.

Wawili hao walichumbiana kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kutengana mwaka uliopita baada ya  Sarah kugundua kuwa  Harmonize alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwigizaji Fridah Kajala.

Harmonize pia alifichua kuwa alikuwa na binti kwa jina Zulekha ambaye Sarah hakuwa na ufahamu wowote kumhusu. Hapo akaamua kumtema mwanamuziki huyo. 

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize amekiri kuwa hiyo ndio sababu wakatengana ila akasema kuwa angeonekana mjinga iwapo angeendelea kumficha mtoto wake.

"Samahani ndilo neno pekee naweza tumia kwa mwanamke huyu mrembo   👩 Alienipatia Miaka (4) Ya maisha Yake Nami Nikampatia (4) Yangu Tulipitia Mengi Ila itoshe Kusema Nilizingua Sanaa ..!!! Mpaka Mungu Alipoamua Kuniletea Mtoto Wangu wa Kwanza @zuuh_konde Na Ndo Ikawa Mwisho Wa Safari Yetu Ya Pamoja. Naaam KUTELEZA KUNATOKEA Naa Muungwana Huomba Radhi 🙏 ila Ningeonekana Mjinga Zaidi Ningeendelea Kumficha Mtoto Wangu" Alisema Harmonize.

Kwenye wimbo huo uliojawa na hisia, Harmonize amekiri kuwa alikuwa amemficha mtoto huyo wake wa kwanza kwa kipindi cha miezi saba.

"Nimekuwa nikificha binti wangu kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, huo ni wazimu! nakupenda sana binti wangu popote ulipo" Harmonize alisema.

Akiomba msamaha kwenye wimbo huo Harmonize alieleza kuwa yeye ni binadamu asiyekamilika na ni kawaida kwa binadamu kukosa.