"Kwa sasa keki ni yake peke yake" Akothee afichua kipenzi chake kipya

Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa anatazamia kupata watoto wawili na mpenzi wake mpya.

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amedai kuwa anampenda Oaks hadi kifo na anaamini kuwa pia yeye anampenda.

•Msanii huyo pia amekiri kuwa aliacha manyumba yake makubwa na kuhamia kwa Oaks.

•Aliwakosoa wale wanaomkashifu kwa kuweka mahusiano yake wazi akisema kuwa wengine wanachumbia watu ambao wameolewa, waliofiwa na wenzao na wengine wazee kuwaliko ndio maana wanaogopa kuyatangaza hadharani kama yeye.

Akothee na Nelly Oaks
Akothee na Nelly Oaks
Image: INSTAGRAM

Ni dhahiri kuwa mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu kama Akothee na aliyekuwa meneja wake Nelly Oaks wanachumbiana..

Siku za hivi karibuni mwanamuziki huyo amekuwa akipakia picha  na video zake wakiwa pamoja na Bw Oaks kwenye mtandao wa Instagram na kuziambatanisha na jumbe zenye kuashiria hisia za mapenzi na kuibua mdahalo mkubwa mitandaoni ila kwa sasa ameamua kuweka wazi kuwa ni kweli wanachumbiana.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amedai kuwa anampenda Oaks hadi kifo na anaamini kuwa pia yeye anampenda.

"Mapenzi ni kitu nzuri sana. Yeye ndiye mwanaume aliye maishani mwangu kwa sasa. Wengine ni wa awali na waliacha vitu ambavyo tunagawana. Kwa sasa keki ni yake na yake peke yake. Acha kusukuma maisha yako ukutani. Nelly Oaks yumo maishani mwangu sasa"Akothee alisema.

Msanii huyo pia amekiri kuwa aliacha manyumba yake makubwa na kuhamia kwa Oaks.

"Kufeli kwa mahusiano yangu ya hapo awali hakumaanishi kuwa sitawahi kuwa na mchumba" Aliendelea kusema.

Mama huyo wa watoto watano amesema kuwa anatazamia kupata watoto wawili na mpenzi wake mpya.

"Napata watoto wawili naye hivi karibuni na akiniacha pia yeye atakuwa kwenye orodha ya 'baby daddies' wangu. Bado nitampatia mapenzi na heshima kama wengine walioniacha," alisema

Aliwakosoa wale wanaomkashifu kwa kuweka mahusiano yake wazi akisema kuwa wengine wanachumbia watu ambao wameolewa, waliofiwa na wenzao na wengine wazee kuwaliko ndio maana wanaogopa kuyatangaza hadharani kama yeye.

"Kwa sababu mko na wapenzi wengi mnafikiria kila mtu ni kama nyinyi? Wengine mko na wanaume wa kulipa nyumba, kulipa uber na wa kununua chakula. Kwangu sina wengi, nachumbia mwanaume mmoja kwa wakati. Nitaendelea kupakia bae wangu hapa hadi siku ile atasema  kuwa hanitaki halafu nitatafuta mwingine" Akothee alisema.

Hivi majuzi mwanamuziki huyo wa miaka 40 alimlaki nchini baba wa kitindamimba chake (Prince Oyoo) ambaye ni Mfaransa pamoja na wanawe wawili Prince Oyoo na Prince Ojwang wanaoishi naye.

Alipokuwa anawalaki alimbubujikia sifa Dominic (Baba Oyoo) na kumshukuru kwa kukubali kumsaidia kulea watoto wake.