Hongera! Hamo na Jemutai waanza ujenzi wa nyumba yao katika juhudi za kuishi pamoja

Wawili hao walifanya hafla ya 'ground breaking' siku ya Jumanne

Muhtasari

•Baada ya kufanikiwa kununua shamba pamoja wiki iliyopita, wacheshi-wapenzi profesa Hammo na Jemutai wameanza shughuli ya ujenzi wa nyumba yao

•Jumanne wiki iliyopita Hamo alitangaza kuwa alikuwa na mpango wa kumjengea nyumba mpenzi wake Jemutai katika juhudi za kuimarisha ndoa yao

Wapenzi Hamo na Jemutai waanza shughuli ya ujenzi wa nyumba yao
Wapenzi Hamo na Jemutai waanza shughuli ya ujenzi wa nyumba yao
Image: HOMES BY SUNG

Baada ya kufanikiwa kununua shamba pamoja wiki iliyopita, wacheshi-wapenzi profesa Hammo na Jemutai wameanza shughuli ya ujenzi wa nyumba yao.

Wawili hao walifanya hafla ya 'ground breaking' siku ya Jumanne kama hatua ya kwanza ya ujenzi wa nyumba yao.

Hammo alitangaza habari za hafla hiyo iliyohudhuriwa na marafiki wachache kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Shughuli ya ujenzi wa nyumba yao itaendelezwa na kampuni ya ujenzi ya Homes By Sung.

Jumanne wiki iliyopita Hamo alitangaza kuwa alikuwa na mpango wa kumjengea nyumba mpenzi wake Jemutai katika juhudi za kuimarisha ndoa yao.

Mcheshi huyo alisema kuwa ingawa hapo awali uhusiano wao umekabiliwa na changamoto si haba, hatua ya kununua shamba ilikuwa mwanzo tu wa kazi inayoendelea na anatazamia kuleta familia yake pamoja ili kuishi kwa furaha.

"Najua tumepitia mengi ila haijalishi tulivyoanza ila tutakavyomalizia. Ilikuchukua muda kuamini kuwa nilitaka familia yangu kuwa pamoja na kuishi kwa furaha, hiyo ni kazi ambayo inaendelea na huu ni mwanzo tu. Naweza kujengea nyumba bila shaka utaifanya kuwa nyumbani " Hamo alisema.

Hatua ya wawili hao kujenga nyumba pamoja inadhihirisha kuwa hata baada ya kutumbuiza wanamitandao na drama za mapenzi miezi kadhaa iliyopita, wacheshi hao wawili waliweza kusuluhisha mzozo uliokuwa baina yao na kwa sasa wako tayari kupeleka uhusiano wao kwenye hatua nyingine.