"Kazi yangu ni kula matunda tu" Ringtone Apoko adai kuwa maumivu yamekithiri mwilini baada ya kupigwa

Mwanamuziki huyo pia aliwaomba mashabiki wake kote Afrika Mashariki kumtumia matunda akidai kuwa hana uwezo wa kula chakula kingine ila matunda tu.

Muhtasari

•Mwanamuziki Ringtone Apoko ameshukuru  mashabiki wake kwa  maombi yao na kuwasihi waendelee kumuombea anapoendelea na safari yake ya matibabu.

•Siku ya Alhamisi msanii huyo aliwasili katika mahakama ya Kibera kushudia mwanablogu Robert Alai akisomewa mashtaka ya shambulio aliyomshtaki nayo. Hata hivyo kesi hiyo haikuendelea baada ya DPP kuitisha tena faili ya kesi hiyo.

Image: INSTAGRAM//RINGTONE APOKO

Mwanamuziki Ringtone Apoko ameshukuru  mashabiki wake kwa  maombi yao na kuwasihi waendelee kumuombea anapoendelea na safari yake ya matibabu.

Kupitia ujumbe aliotoa kupitia ukurasa wake wa Instagram alasiri ya Jumamosi, Apoko amedai kuwa maumivu yamekithiri mwilini wake.

"Nataka kuwashukuru sana kwa kuhusika kwenye safari yangu. Wakenya na wengine Afrika Mashariki nawashukuru kwa kuwa pamoja nami wakati wa maumivu na asanteni kwa kunipenda. Mimi nimeumia, mimi ni mgonjwa naumwa sana lakini nataka kuwashukuru sana kwa maombi." Apoko alisema.

Mwanamuziki huyo pia aliwaomba mashabiki wake kote Afrika Mashariki kumtumia matunda akidai kuwa hana uwezo wa kula chakula kingine ila matunda tu.

"Kazi yangu ni kula tu tumatunda. Ukipata matunda mahali Wakenya, Watanzania, Waganda na Warwanda tafadhali mtumane. Mungu atanisaidia. Tumatunda tu nitakula" Ringtone alisema.

Siku ya Alhamisi msanii huyo aliwasili katika mahakama ya Kibera kushudia mwanablogu Robert Alai akisomewa mashtaka ya shambulio aliyomshtaki nayo. Hata hivyo kesi hiyo haikuendelea baada ya DPP kuitisha tena faili ya kesi hiyo.

Ringtone ambaye alionekana kuwa na maumivu  aliwasili mahakamani akiwa amebebwa na gari la kubebea wagonjwa.

Msanii huyo aliyekuja kutambulikana sana kutokana na kibao chake 'Pamela' alikuwa na bendeji mkononi na kwenye kidevu chake.

Alipokuwa anahutubia wanahabari nje ya mahakama, mwanamuziki huyo alidai kuwa alikuwa na maumivu tele kwenye kichwa na mkono wake na alikuwa ametoka hospitani baada ya kulala huko.

"Mimi naumwa! Mwili wangu hauko sawa. Mimi sikuwa mgonjwa" Ringtone alidai.

Image: INSTAGRAM//RINGTONE APOKO

Msanii huyo alisema kuwa hakuwa ametenda kosa lolote dhidi ya Alai wakati aliamua kumshambulia kwa rungu.

"Mimi sikumkosea Robert Alai na aliamua tu kunivamia. Nilipandisha kioo ya gari wakati alikuja kunitukana. Yeye akaona akuje na rungu apasue kioo ya gari. Akavunjavunja na akanifikia na akaniumiza," Aliendelea kusema.

Alihimiza taasisi za kulinda sheria kuhakikisha kuwa sheria imefuatwa kila wakati.

"Ile siku mimi Ringtone nitaenda nivamie mtu, nataka tu sheria itumike... nashangaa kwa nini kesi yangu inaendelea tu kuzungushwa.. Nataka kuambia Wakenya wa kawaida tusipoteze matumaini. Bado naamini Kenya ni nchi ambayo ninafuata sheria, ata kama ni mtu mkubwa ama mdogo, ukikosea mwenzako kwa kumpiga lazima sheria itatumika" Alisema Ringtone.