"Msalimie mama" Diana Marua amwomboleza nyanyake aliyechukua jukumu la mama kwa ujumbe wa kihisia

Marua amesema kuwa nyanyake ambaye aliaga siku ya Ijumaa ndiye alichukua majukumu ya marehemu mama baada ya kutokuwepo tena kwa mamake mzazi

Muhtasari

•Diana Marua ambaye ni mke wa mwanamuziki maarufu nchini Kevin Bahati ameomboleza kifo cha nyanya yake mpendwa

•Marua amesema kuwa nyanyake ambaye aliaga siku ya Ijumaa ndiye alichukua majukumu ya marehemu mama baada ya kutokuwepo kwa mamake mzazi.

Image: INSTAGRAM//DIANA MARUA

Diana Marua ambaye ni mke wa mwanamuziki maarufu nchini Kevin Bahati ameomboleza kifo cha nyanya yake mpendwa.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram Marua amepakia video inayoonyesha akiwa anapiga gumzo na  marehemu nyanyake wakati alikuwa akipokea matibabu hospitalini na kuambatanisha na ujumbe wa kihisia.

Marua amesema kuwa nyanyake ambaye aliaga siku ya Ijumaa ndiye alichukua majukumu ya marehemu mama baada ya kutokuwepo kwa mamake mzazi.

"Jana  niliamkia habari za kusikitisha kuwa Mungu amemchukua mtu wa thamani sana maishani mwetu.Shosho ulinifanyia kila kitu wakati sikuwa na mahali pa kwenda. Ulichukua majukumu ya mama wakati hakuwa tena na kwa hayo nitaishi kushukuru" Marua aliandika.

Diana amekiri kuwa kwa kipindi cha miezi miwili ambacho nyanyake alikuwa amelazwa hospitalini angelia sana hadi kulala baada ya kumtembelea na kutazama alivyokuwa na maumivu.

"Uliteseka sana kwa kipindi cha miezi miwili ambayo ulikuwa hospitalini. Ningeendesha gari  kurudi nyumbani nikiwa nalia kutoka hospitalini. Nililia hadi kulala, maumivu yalikuwa mengi singeweza kustahimili. Singeweza kuendelea tena" Alisema Diana.

Amesema kuwa walijaribu kadri ya uwezo wao kuhakikisha kuwa nyanya yake amepata matibabu na kuwa na imani kuwa angepona.

Mama huyo wa watoto wawili amesema kuwa anafurahi kwa kuwa  kutoka sasa nyanyake hateteseka tena kwa sababu ya maumivu.

"Nina amani sasa kuwa hauna maumivu tena. Naahidi kuwa nitaendelea kukufanya ufurahie" Alisema

"Salimia mama. Naahidi kuwa nitaendelea kuwafanya mfurahi" Alimalizia kwa kusema.

Diana ambaye ni mzaliwa wa Nyanza alipoteza mama yake mzazi zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Wanamitandao wengi wamejumuika kumfariji Marua kufuati hayo.