'Nilikula colgate kama chajio' Robert Burale asimulia jinsi matatizo yalimshinikiza kujitoa uhai mara tatu

Burale ambaye anatambulika sana kwa kupeana motisha amekiri kuwa amejaribu kujitoa uhai nyakati tatu tofauti wakati maisha yalikuwa yamempiga chenga.

Muhtasari

•Akiwa kwenye mahojiano na Daniel Ndambuki katika kipindi cha Churchill Show, Burale amesema kuwa ugumu wa maisha ulimshinikiza kujaribu kitendo hicho mara moja alipokuwa akisomea Uingereza na mara mbili akiwa humu nchini.

•Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 44 amesema kuwa kwa wakati mmoja hali ngumu ya maisha na njaa ilimsukuma kula dawa ya meno kama chakula cha jioni.

Image: INSTAGRAM//ROBERT BURALE

Mhubiri mahuhuri nchini Robert Burale amefunguka kuhusu nyakati ngumu maishani mwake zilizomshinikiza kutaka kujitoa uhai.

Burale ambaye anatambulika sana kwa kupeana motisha amekiri kuwa amejaribu kujitoa uhai nyakati tatu tofauti wakati maisha yalikuwa yamempiga chenga.

Akiwa kwenye mahojiano na Daniel Ndambuki katika kipindi cha Churchill Show, Burale amesema kuwa ugumu wa maisha ulimshinikiza kujaribu kitendo hicho mara moja alipokuwa akisomea Uingereza na mara mbili akiwa humu nchini.

"Kusema kweli sikuwa tu na mawazo ya kujitoa uhai, nilijaribu kujitoa uhai. Kuna tofauti, watu wengi wana mawazo ya kujitoa uhai. Mimi nimejaribu mara tatu.. UK nilijaribu, mara mbili huku. Maisha ilikuwa ngumu" Burale alisema.

Mhubiri huyo mwenye umri wa miaka 44 amesema kuwa kwa wakati mmoja hali ngumu ya maisha na njaa ilimsukuma kula dawa ya meno kama chakula cha jioni.

"Maisha ilikuwa ngumu hata singeweza kugharamia milo tatu kwa siku. Unajua nimewahi kula dawa ya meno kama chajio, sio kwa sababu za  usafi" Alikiri Burale.

Alisema alisema kuwa kwa wakati huo alipokuwa anateseka  hakuwa na yeyote wa kumsaidia kwani watu wengi walimtoroka. Hata hivyo alisema kuwa jambo hilo lilimsaidia kujijenga kimaisha.

"Wakati mwingine Mungu akitaka upitie msimu fulani atafunga njia zote za usaidizi. Namshukuru sana Mola kuwa watu wengi walinitoroka kwani ilinijenga kuwa mtu nilye kwa sasa. Hakuna ambaye anaweza kuja kwangu kwa sasa aniambia hajakula na nimnyime chakula" Aliendelea kusema.

Burale alidai  kuwa anafahamu vyema kuwa njaa yaweza kumfanya mwanaume mzima kulia kwani pia yeye amepitia pale.