"Mamangu alikuwa mgeni kwa dadangu" Diana Marua azungumzia maisha magumu utotoni baada ya wazazi wake kutengana

Diana amesema kuwa alikuwa katika darasa la pili wakati mama yao aliwaacha ilhali dada yake mdogo Michelle alikuwa na umri wa miezi tisa tu

Muhtasari

•Kupitia mtandao wa YouTube, Diana amesema kuwa yeye pamoja na dada zake wadogo, Varl na Michelle  walilelewa na baba yao pekee yake baada yake kutengana na mama yao wakiwa na umri mdogo sana.

•Diana ameeleza kuwa Michelle hakuwa anamfahamu mama yao na yeye ndiye alichukua jukumu la kumtambulisha kwake.

Image: INSTAGRAM//DIANA MARUA

Diana Marua ambaye ni mke wa mwanamuziki mashuhuri Kevin Bahati amefunguka kuhusu maisha magumu ya utotoni ambayo alipitia pamoja na dada zake wawili baada ya kutengana kwa wazazi wake.

Kupitia mtandao wa YouTube, Diana amesema kuwa yeye pamoja na dada zake wadogo, Varl na Michelle  walilelewa na baba yao pekee yake baada yake kutengana na mama yao wakiwa na umri mdogo sana.

Diana amesema kuwa alikuwa katika darasa la pili wakati mama yao aliwaacha ilhali dada yake mdogo  Michelle alikuwa na umri wa miezi tisa tu.

Mwanavlogu huyo amefichua kuwa ilimchukua Michelle muda kumtambua mama yao kwani aliachwa akiwa mdogo mno. Amesema kuwa mama yao angewatembelea mara kwa  mara baada ya kipindi kirefu.

"Nakumbuka kuwa mama yangu alikuwa akitutembelea baada ya kipindi kirefu. Hiyo ingekuwa hata mara moja tu kwa kipindi cha miezi mitatu ama kipindi kirefu kama miezi sita. Nakumbuka kuna nyakati tulikuwa tunamkimbilia wakati tulimuona akija. Tulimkuwa tunamkimbilia na kumkumbatia" Diana alisimulia.

Diana ameeleza kuwa Michelle hakuwa anamfahamu mama yao na yeye ndiye alichukua jukumu la kumtambulisha kwake.

"Nakumbuka kuna wakati mmoja ambapo Michelle aliona mama yetu na alikuwa anajificha nyuma yangu na nikamuuliza, 'Michelle nini mbaya? Nenda kamkumbatie.' Na akawa anajiuliza mbona tulikuwa tunamkimbilia na kwani yeye ni nani., unajua aliachwa akiwa mdogo sana. Na nakumbuka nikimwambia kuwa huyo ndiye mama. Hapo ndipo akamkimbilia na kumkumbatia." Diana alieleza.

Alisema kuwa aliendelea kufahamisha dada yake kuhusu mama yao ili aweze kumkubali ila aikuwa rahisi kwani alikuwa mgeni kwani

Diana alisema kuwa kutengana kwa wazazi wake kulimlazimu kukomaa mapema kimawazo ili aweze kulea watoto wao.

"Ilibidi nikomae haraka kimawazo. Ilinilazimu nifanye maamuzi, nililazimika kuangalia dada zangu wadogo na kujua kupika, kufua nguo na kujifunza kufanya kila kitu nyumbani. Nakumbuka dada zangu walikuwa wakilia sana mbona mama yetu hakutufanyia haki na kwa nini hakuwa akitutembelea. Kulikuwa na utupu ndani yake na ningejua" Marua aliendelea kusema.

Alisema kuwa dada yake Michelle alipitia wakati mgumu haswa shuleni wakati alikuwa akiskia watoto wenzke wakizungumza kuhusu mama zao.