"Wewe ni kila kitu nilichoomba" Diana Marua ashukuru Bahati kwa kumzawadi gari pamoja na wanawe

Bahati alimweleza mkewe Diana Marua kuwa kazi ya gari lile haswa itakuwa kuwapeleka watoto wao shule wakati hawatajiskia kuabiri basi la shule.

Muhtasari

•Alfajiri ya Jumanne familia ya msanii huyo iliamkia zawadi ya gari aina ya Mercedes W205 kutoka kwake.

•Diana alimshukuru sana mumewe na akamshukuru Mola pia kwa kumpa mume wa ndoto zake

Image: INSTAGRAM//DIANA MARUA

Mwanamuziki mashuhuri Kelvin Bahati almaarufu kama 'mtoto wa mama' ameendelea kuwapa wanaume wengine changamoto ya jinsi ya kutunza wapenzi wao.

Alfajiri ya Jumanne familia ya msanii huyo iliamkia zawadi ya gari aina ya Mercedes W205 kutoka kwake.

Bahati alitumia mtandao wa YouTube kuonyesha mashabiki wake hali ilivyokuwa akishangaza familia yake na zawadi hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Bahati alimweleza mkewe Diana Marua kuwa kazi ya gari lile haswa itakuwa kuwapeleka watoto wao shuleni wakati hawatajiskia kuabiri basi la shule.

"Babe nafurahia kuwa ulifurahia zawadi yangu ndogo kwako na watoto. Pokea Mercedes W205 haswa ya kupeleka watoto shule wakati hawatajiskia kutumia basi la shule. Nakupenda" Bahati alisema.

Kwa upande wake Diana alieleza furaha yake na mapenzi makubwa kwa mumewe baada kupokea zawadi hiyo maalum.

Diana alimsifia sana mumewe na kusema kuwa yeye ni kila kitu ambacho alimuomba Mungu.

"Wewe ni kila kitu ambacho niliomba na hadi kikaongezewa kachumbari juu yake. Mimi na watoto wangu tuliamkia gari mpya aina ya Mercedes Benz W205  kutoka kwa mume wangu. Nimejawa na raha sana." Diana aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Alimshukuru sana mumewe na akamshukuru Mola pia kwa kumpa mume wa ndoto zake.

Bahati alimjibu Diana kwa kusema kuwa hiyo ilikuwa 'toy' ndogo yake na watoto.

"Ni 'toy' ndogo tu yako na watoto" Bahati alisema.