'Aibu kwenu!' Vera Sidika awakemea wanaomkejeli na kumtusi juu ya mabadiliko mwilini yaliyotokana na ujauzito

Vera amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa pia wanawake ambao ambao wamewahi kupitia safari ile ya ujauzito wako katika mstari wa mbele kumtusi

Muhtasari

• Mama huyo mtarajiwa amesema kuwa kunao baadhi ya wanamitandao haswa wanawake ambao wamekuwa wakimtania kufuatia mabadiliko ambayo yameanza kujitokeza mwilini.

•Kulingana na mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 31, wanawake ndio maadui wakubwa wa wanawake wenzao.

VERA SIDIKA NA MPENZIWE BROWN MAUZO
VERA SIDIKA NA MPENZIWE BROWN MAUZO
Image: INSTAGRAM

Mwanasoshalaiti Vera Sidika amewakosoa wanaomtania na kumkejeli kufuatia mabadiliko mwilini wake yanayotokana na ujauzito wake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo mtarajiwa amesema kuwa kunao baadhi ya wanamitandao haswa wanawake ambao wamekuwa wakimtania kufuatia mabadiliko ambayo yameanza kujitokeza mwilini.

Vera amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa pia wanawake ambao ambao wamewahi kupitia safari ile ya ujauzito wako katika mstari wa mbele kumtusi

Kulingana na mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 31, wanawake ndio maadui wakubwa wa wanawake wenzao.

"Wengine wenu haswa wanawake mnafaa kufanya bora zaidi . Wanawake ndio adui wakubwa kwao wenyewe. Bure kabisa.

Wengine wenu hata hamngeweza kutoka kitandani wakati mlikuwa wajawazito wala kuvaa nguo, kujipondoa, kuenda mahali ama kufanya kazi yoyote.

Wengine wenu wamekuwa kwenye safari ya ujauzito kama mimi na  wao ndio wa kwanza kurusha mawe na kuniita majina mabaya kwa sababu ya mabadiliko usoni mwangu. Nani aliwaumiza?" Vera aliandika.

Aliendelea kusema kuwa wale wanaomshambulia mitandaoni hawakuwa na ujasiri kama wake wakati wao walikuwa wajawazito.

"Tuonyeshe sura zenu wakati mlikuwa wajawazito. Wengine wenu hata hamkupiga picha yoyote kwa sababu hamkuwa na ujasiri kufuatia mabadiliko mlioshuhudia. Na nyinyi ndio wa kwanza kushambulia mtu ambaye ana ujasiri wa kutembea na kuonyesha kila kitu katika safari yake ya ujauzito" Vera alisema.

Vera amesema kuwa licha ya maneno mabaya na matusi anayopokea ataendelea kupakia picha zake na video za safari yake ya ujauzito.

"Hata kama utasema nakaa kama mwanaume, mbuzi ama ngombe nitanendelea kupakia picha na video. Ni uso wangu na  mwili wangu uliobeba baraka. Sio wenu.Mnikome na chuki mjaribu mwaka ujao kwani napanga kupata ujauzito mara ingine na ingine hadi nichoke. Mtazoea tu" Alisema.

"Wengine wenu mnakaa vibaya hata mkiwa mmejipondoa sana lakini mmejipa kazi ya kushambulia mwanamke mjamzito ambaye hajajipondoa. Aibu kwenu. Tuonyeshe nyuso zenu" Vera alisema.