"Niko single kabisa na sitafuti mtu" Amber Ray athibitisha kuvunjika kwa ndoa yake na Jamal Rohosafi

Licha ya kuvunjika kwa ndoa yake na Jamal, Amber Ray ameapa kuwa bado hajapoteza matumaini yake kwa ndoa

Muhtasari

•Akiwa kwenye kipindi cha maswali na majibu katika mtandao wa Instagram, Amber Ray amedai kuwa ako 'single' na hatafuti mchumba kwa sasa.

•Alipoulizwa na shabiki mwingine ikiwa ana nia ya kuolewa tena, Amber Ray alisema kuwa ataendelea kujaribu ndoa tena na tena mpaka siku itamkubali.

Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mwanasoshalaiti maarufu Faith Makau almaarufu kama Amber Ray amethibitisha wazi kuwa kwa sasa hachumbiani na yeyote.

Akiwa kwenye kipindi cha maswali na majibu katika mtandao wa Instagram, Amber Ray amedai kuwa ako 'single' na hatafuti mchumba kwa sasa.

"Mimi niko 'single' kabisa na sitafuti.. sitaki mtu" Amber Ray alidai.

Mama huyo wa mtoto mmoja alikuwa anamjibu shabiki wake aliyetaka kujua ikiwa bado anachumbiana na mfanyibiashara Jamal Marlow Rohosafi.

Hii ni dhihirisho wazi kuwa bila shaka wapenzi hao wawili wametengana kabisa baada ya kuchumbiana kwa kipindi cha miezi kadhaa tu.

Kwa kipindi, Amber Ray alikuwa ameolewa kama mke wa pili na Jimal Rohosafi ambaye ni mfanyibiashara mashuhuri sana jijini Nairobi na wawili hao hawakuficha mapenzi yao hadharani.

Hata hivyo, mwezi uliopita dalili kuwa ndoa kati yao ilikuwa imevunjika zilianza kuonekana haswa wakati Amber Ray aliondoka kutoka nyumbani kwake alikokuwa akiishi na Jamal upande wa Syokimau.

Licha ya kuvunjika kwa ndoa yake na Jamal, Amber Ray ameapa kuwa bado hajapoteza matumaini yake kwa ndoa.

Alipoulizwa na shabiki mwingine ikiwa ana nia ya kuolewa tena, Amber Ray alisema kuwa ataendelea kujaribu ndoa tena na tena mpaka siku itamkubali.

"Hii kitu nang'ang'ana nayo mpaka siku itakubali" Amber Ray amedai.