"Nitaacha muziki!" mwanamuziki Willy Paul aapa iwapo albamu yake haitafaulu

Willy Paul amedai kuwa amewekeza pesa, wakati na nguvu zake nyingi kutengeneza albamu hiyo na haoni kama inaweza kufeli.

Muhtasari

•Siku za hivi karibuni mwanamuziki huyo ambaye aligura injili takriban miaka miwili iliyopita amekuwa akijinata na kudai kuwa ametengeneza albamu moto zaidi ya albamu za wasanii wengine nchini.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Mwanamuziki matata nchini Wilson Abubakar Radido almaarufu kama Willy Paul ameapa kuwa ataacha muziki iwapo albamu anayotazamia kuachilia hivi karibuni haitaafikia makadirio yake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul amedai kuwa anaamini kuwa albamu yake ni bora zaidi kuliko albamu ambazo zimetolewa na wanamuziki wengine nchini hapo awali.

Paul amedai kuwa amewekeza pesa, wakati na nguvu zake nyingi kutengeneza albamu hiyo na haoni kama inaweza kufeli.

"Kama mnavyojua, niko na albamu ambayo inakuja na iwapo haitabadili maisha yangu na kubadili jinsi watu wanavyonitazama, nitaacha muziki. Naamini kuwa nimewekeza wakati na nguvu nyingi kutengeneza albamu hii. Nimejitolea kila kitu yangu kwa hivyo iwapo haitafanya kazi basi nitaacha muziki, sina shaka na hayo, heri tu ifanye kazi.. Kweli kuna wanamuziki wametoa albamu hapo awali ila naamini hakuna kama hii.. narudia, kama haitafanya kazi basi nitaacha muziki" Willy Paul amesema.

Siku za hivi karibuni mwanamuziki huyo ambaye aligura injili takriban miaka miwili iliyopita amekuwa akijinata na kudai kuwa ametengeneza albamu moto zaidi ya albamu za wasanii wengine nchini.