Staa wa Bongo Harmonize apanga kuzindua stesheni yake ya redio na ya TV

Harmonize ameonekana kuiga mfano wa Diamond ambaye tayari anamiliki Wasafi TV na Wasafi FM, stesheni ambazo zinavuma sana Bongo na kote Afrika Mashariki.

Muhtasari

•Siku ya Jumamosi, mwanamuziki huyo alifahamisha mashabiki wake kuwa ako katika harakati za kuanzisha kampuni yake ya vyombo vya habari itakayojumuisha stesheni ya redio na televisheni.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize anaendelea kupiga hatua  kubwa kwenye ulingo wa sanaa kila uchao licha ya kulelewa katika hali duni.

Harmonize ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa Konde Gang Worlwide ameonekana kufuata nyayo za bosi wake wa hapo awali akiwa Wasafi, Diamond Platnumz almaarufu kama simba kwenye sanaa huku akitazamia kuwa msanii bora Bongo.

Siku ya Jumamosi, mwanamuziki huyo alifahamisha mashabiki wake kuwa ako katika harakati za kuanzisha kampuni yake ya vyombo vya habari itakayojumuisha stesheni ya redio na televisheni.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Harmonize alichapisha ujumbe ambao uliashiria kuwa mradi wake wa kuanzisha Kondegang FM na Kondegang TV ulikuwa umekamilika na huenda akauzindua hivi karibuni.

"Kondegang FM na Kondegang TV, 100% usiku wa leo... Mungu ni mwema" Harmonize aliandika.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Kufuatia hatua hii Harmonize ameonekana kuiga mfano wa Diamond ambaye tayari anamiliki Wasafi TV na Wasafi FM, stesheni ambazo zinavuma sana Bongo na kote Afrika Mashariki.

Harmonize alikatiza uhusiano wake na Diamond na kugura Wasafi mwaka wa 2019 na tangu wakati huo amekuwa akichapa shughuli zake kivyake. Ameweza kuanzisha 'label' inayofahamika kama Konde Music Worldwide na tayari amesajili wasanii kadhaa.