"Tangu mke mwenza aolewe, mume wangu amekuwa mbali na mimi" Mke wa kwanza wa Omosh asimulia ndoa yake ilivyosambaratika

Amedai kuwa mumewe hawajibikii familia yake tena na licha yake kupata usaidizi mkubwa kutoka kwa Wakenya ikiwemo kujengewa nyumba hajampa usaidizi wa namna yoyote.

Muhtasari

•Wacuka amekiri kuwa ndoa yake na Omosh ilianza kuyumba takriban miaka kumi iliyopita wakati mwigizaji huyu maarufu aliamua kuoa mke wa pili.

•Amekiri kuwa bado anampenda mumewe na anampeza sana kwani yeye bado ni baba ya watoto wake ila haoni kama yeye anampenda.

Image: SCREENSHOT// KAMUHUNJIA YOUTUBE

Mwigizaji Judy Wacuka almaarufu kama Mrs Ngatia amefunguka kuhusu uhusiano wake na mumewe Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh.

Akizungumza na Hiram Maina kupitia mtandao wa YouTube, Wacuka amekiri kuwa ndoa yake na Omosh ilianza kuyumba takriban miaka kumi iliyopita wakati mwigizaji huyu maarufu aliamua kuoa mke wa pili.

Wacuka ameeleza kuwa uhusiano wao haujakuwa wa  kujivunia kwani Omosh alijitenga naye na kuwekeza wakati wake wote kwa mke wa pili.

"Tangu aolewe, baba ya watoto wangu amekuwa mbali sana na mimi. Vile mwanamke anaweza tamani mumewe  awe karibu na yeye, baba ya watoto wangu amekuwa mbali sana na mimi. Ninapomtaka  nikitaka kumwambia kuhusu watoto ama kitu kingine nachukua tu simu nampigia.. ninapompigia ananiambia kuwa atakuja lakini hatimizi. Inabidi nishike njia niende huko wanakoishi na mke mwenzangu" Wacuka alisema.

Mama huyo wa watoto watatu amesema kuwa mumewe huwa hampatii muda wake na kukiri kuwa kamwe hafurahii maisha ya upweke.

Amedai kuwa mumewe hawajibikii familia yake tena na licha yake kupata usaidizi mkubwa kutoka kwa Wakenya ikiwemo kujengewa nyumba hajampa usaidizi wa namna yoyote.

"Amekaa mbali na mimi, hana muda na mimi, anakaa mbali na watoto wangu. Anatumia jina langu na watoto wangu kuomba usaidizi ambao hanipatii" Wacuka alieleza.

Hata hivyo, Wacuka amesema kuwa bado anamtambulisha Omosh kama mumewe kwani hajawahi kumwambia wazi kuwa hamtaki tena. Amesema kuwa bado anampenda mwigizaji huyo

"Hajawahi niambia mbele ya watu kuwa  hanitaki. Hajawahi enda kwa wazazi wangu akawaambia kuwa amerudisha msichana wao kwani hamtaki tena. Mimi nashangaa mimi ni mke wa nani.. watoto wangu wanampeza baba yao. Hana wakati na mimi na hata hataki kujua tunayoyapitia... nashindwa niko wapi, hajawahi niambia kuwa amenitupa" Alisema.

Alisema kuwa anasikitika kuona kuwa Omosh humtambulisha kama mke wake wa kwanza na mama ya watoto wake watatu kila anakoenda ila hawajibikii familia  hiyo anapopata msaada.

"Akienda mahali popote anaambia watu kuwa mimi ni mke wake na watoto wangu ni wake lakini hajawahi kuniambia kuwa ameniacha ndivyo aniachilie. Inakaa ni kama amenifunga kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita... Hajawahi kuniambia nitoke eti amenitupa. Ananichukia tu bure, hajawahi kunisaidia... Mimi nashnagaa mbona alitumia jina langu na watoto wangu kuomba msaada kwa Wakenya na msaada ilipatianwa  watu wakifikiria  tuko pamoja. Hatuko pamoja" Wacuka alisema.

Wacuka amesema kuwa ingawa ndoa yake ilibadilika baada ya Omosh kuoa mke mwingine, hana ugomvi wowote na mke mwenzake na anamheshimu sana.

Amekiri kuwa bado anampenda mumewe na anampeza sana kwani yeye bado ni baba ya watoto wake ila haoni kama yeye anampenda.

"Nampenda Omosh, lakini yeye hajawahi kunipenda. Nampenda na nampeza sana.. nakumbuka enzi zile, Omosh alikuwa mzuri sana na alikuwa mwenye mapenzi. Nampenda bado kwani yeye ndiye baba ya watoto wangu na hakutatokea mwingine aseme yeye ndiye baba ya watoto wangu na Omosh ndiye baba yao.Mimi nampenda lakini hana wakati na mimi" Wacuka alisema.

Wacuka alifichua kuwa walikaa na Omosh kwa kipindi cha miaka 18 kabla ya kutengana kwao miaka 10 iliyopita wakati mke wa pili aliletwa.