Juliani atishiwa maisha baada ya kuvunja kimya kuhusu uhusiano wake na aliyekuwa mke wa gavana Mutua

Msanii huyo alimalizia kwa kumuagiza anayemtishia asiharibu sura yake kwani angependa kuzikwa akiwa anatabasamu

Muhtasari

•Juliani alifichua kwamba alipata vitisho kwenye simu yake baada ya kuvunja kimya kuhusu uhusiano wake na Bi Lilian

Image: INSTAGRAM// LILIAN NG'ANG'A

Siku ya Jumatano mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani alijitokeza kuzungumzia madai kuwa anachumbia aliyekuwa mke wa gavana Alfred Mutua Bi Lilian Ng'ang'a.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, msanii huyo alichapisha ujumbe wa kimafumbo na kusema kuwa watu wana uhuru wa kufikiria wanavyotaka.

Baba huyo wa mtoto mmoja aliyepata na aliyekuwa mpenzi wake mwigizaji Brenda Wairimu alisema kuwa hakuna haja yake kutoa taarifa kuhusu jambo ambalo ni wazi.

"Asante sana kwa wale ambao wamewasiliana nami ndani ya kipindi cha wiki chache zilizopita. Mola awazidishie.

Hakuna haja ya kutoa taarifa kuhusu suala ambalo ni wazi. Najua mnaweza jiwazia wenyewe. Pateni hitimisho wenyewe. Nawaaminia" Juliani aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Masaa machache baada ya kuandika ujumbe huo, mwanamuziki huyo anayefahamika zaidi kutokana na nyimbo zake 'Utawala' na 'Niko njaa' alichapisha ujumbe mwingine wa kuhofisha akieleza vitisho dhidi ya maisha yake.

Juliani alifichua kwamba alipata vitisho kwenye simu yake baada ya kuvunja kimya kuhusu uhusiano wake na Bi Lilian.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa simulizi ya kunyang'anyana mke ni jambo la uongo na kusema kuwa hakuna vile mtu mzima anaweza 'kuibiwa'

"Unawezaje 'kuiba' mtu? Mtu mzima mwenye akili timamu! "Simu niliyopigiwa na ujumbe wa vitisho dhidi ya maisha yangu ambao nilipata leo sio jambo la kufurahisha! Simulizi ya 'Ulinyang'anyana ni ya uongo, ya kuchokesha na vichwa  tamu vya habari tu. Tafadhali wacheni" Juliani aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Msanii huyo alimalizia kwa kumuagiza anayemtishia asiharibu sura yake kwani angependa kuzikwa akiwa anatabasamu.

"Kwa vitisho, usipime uso, ningependa kutabasamu ndani ya kaburi langu" Juliani alisema.

Tangu Mutua na Lilian watangaze kuvunjika kwa ndoa yao mwezi uliopita uvumi  umekuwa ukitanda mitandaoni kuwa msanii huyo ndiye sababu kuu ya kutengana kwao.

Picha kadhaa  za msanii huyo akijivinjari na Lilian zimekuwa zikienezwa mitandaoni na kusemekana kuwa wamejitosa kwenye uhusiano wa kimapenzi.