'Tafuta kazi uache kuvunja boma za watu' Mwanasoshalaiti Bridget Achieng asherehekea masaibu yanayomkumba Edgar Obare

Muhtasari

•Kulingana na Achieng', kwa muda mrefu Obare amekuwa akiwatia kasumba Wakenya wengi huku akiharibia wengine majina na katika harakati ya kutekeleza hayo akaweka maisha yake na ya familia yake hatarini.

•Mwanasoshalaiti huyo anayedaiwa kutumia milioni 10 kuchumbua ngozi yake takriban miaka miwili iliyopita amesema kuwa Obare hafai kutarajia kuhurumiwa na kuungwa mkono na kila mtu.

Image: INSTAGRAM

Mwanasoshalaiti mashuhuri Bridget Achieng ameonekana kufurahia masaibu yanayomkumba mwanablogu Edgar Obare.

Kipindi kifupi baada ya Obare kutangaza kutekwa nyara kwa ndugu yake na watu waliotaka afichue mahali alipo, Achieng alitumia ukurasa wake wa Instagram kuonyesha kuridhika kwake na tukio hilo huku akisema kwamba mambo ya mwanablogu huyo hayatawahi kuwa sawa kufuatia machungu ambayo amefanya wengine wapitie.

Kulingana na Achieng', kwa muda mrefu Obare amekuwa akiwatia kasumba Wakenya wengi huku akiharibia wengine majina na katika harakati ya kutekeleza hayo akaweka maisha yake na ya familia yake hatarini.

Kufuatia hayo mwanasoshalaiti huyo anayedaiwa kutumia milioni 10 kuchumbua ngozi yake takriban miaka miwili iliyopita amesema kuwa Obare hafai kutarajia kuhurumiwa na kuungwa mkono na kila mtu.

"Unayochapisha kwenye ujumbe wako ni ya kweli, hata kama sio kila mtu atakubaliana nawe. Huwezi haribia watu majina na utarajie kila mtu asimame na wewe. Chapisho nzuri.. Huyu jamaa amewatia kasumba Wakenya wengi, Wah, enyewe udaku haitaki uvivu, unaweka maisha yako na ya familia yako hatarini unufaike na nini?  Mimi nimeshazoea hakuna kitu cha kunivunja tena.. kuongelelewa nayo tulishazoea.. unakula machozi ya watu EDGAR OBARE hutawahi pata amani. Ukitaka andika kunihusu toka leo hadi mwaka ujao, nitakuwa naomba. Hakuna mfuasi wako hata mmoja atakuwepo wakati mabaya yatakufanyikia" Achieng' aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa mtoto mmoja amemwagiza Obare kutafuta kazi ya maana na aache kuvunja boma za wenyewe huku akijiita 'whiste blower' (mtoa habari)

"Kuwa mwenye maarifa na utafute kazi ya kikweli, sio kuvunja boma za wengine ati 'Whistle blower'" Achieng alimwarifu Obare.

Siku ya Jumapili Obare alidai kuwa ndugu yake alitekwa nyara na watu wasiojulikana ambao walitaka kujua mahali alipo. Alihusisha tukio hilo na hatua yake kuchapisha taarifa kuhusu biashara haramu ya 'Wash Wash' inayodaiwa kuendelea nchini