Mwanamuziki Pitson asimulia alivyotemwa na mkewe mara mbili kwa kulipia wanawake nyumba na kulala nao

Alisema kuwa wanawake wote ambao alikuwa anatunza walikuwa wameokoka.

Muhtasari

•Msanii huyo alisema kuwa alipokuwa katika chuo kikuu hakuwahi tania ama kubusu msichana yeyote

•Pitson alisema kwamba kwa kuwa  alikuwa na pesa nyingi kwa wakati huo alikuwa analipia wanawake tofauti kodi ya nyumba na akawa 'sponsor' wao.

•Mwanamuziki huyo alisema kuwa mkewe aligundua tabia yake kwa kuwa hesabu za bajeti yao hazikuwa zinaingiana.

Image: HISANI

Habari na Elizabeth Ngigi

Ndoa ya mwanamuziki wa nyimbo za injili Peterson Ngetha almaarufu kama Pitson  ilikuwa karibu kuvunjika kufuatia tabia yake ya kutunza wanawake na kugharamia mahitaji yao.

Akiwa kwenye mahojiano na Robert Burale kwenye kipindi cha 'Oh Men', Pitson alisema kwamba alipata pesa nyingi baada ya kutoa kibao 'Lingala ya Yesu' ambacho kilivuma sana.

Pitson alifichua kuwa alilelewa na mhubiri.

"Nilikuwa kwa kikundi ambacho msimamo ulikuwa 'ubikira ni nguvu'. Tulikuwa na makubaliano kuwa hakuna kushiriki tendo la ndoa na wapenzi wetu" Pitson alisema.

Msanii huyo alisema kuwa alipokuwa katika chuo kikuu hakuwahi tania ama kubusu msichana yeyote.

"Nilipatana na mke wangu nikiwa mwaka wa pili. Tulianza kuchumbiana na tukafunga ndoa. Baadae nilipata kazi katika benki. Hapo ndipo nilitoa wimbo 'System ya Kapungala'. Kulikuwa na pesa nyingi kwa wakati huo" Pitson alisema.

Alieleza kuwa alikuwa mdogo, na mke ila majukumu yalikuwa kidogo.

"Nilikuwa natengeneza pesa nyingi na nilikuwa naishi kwa nyumba ambayo nilikuwa nalipia kodi ya shilingi 22,000 Kinoo. Pesa ni kama mtumishi, usipoipatia kazi basi italeta utundu" Alisimulia Pitson.

Pitson alisema kwamba kwa kuwa  alikuwa na pesa nyingi kwa wakati huo alikuwa analipia wanawake tofauti kodi ya nyumba na akawa 'sponsor' wao.

"Wangenilipa kwa kulala nao. Usafi na uaminifu ulikuwa umeniondokea. Mke wangu aligundua" Alisema Pitson

Mwanamuziki huyo alisema kuwa mkewe aligundua tabia yake kwa kuwa hesabu za bajeti yao hazikuwa zinaingiana.

"Aliondoka na jambo la kuaibisha ni kuwa wazazi wangu walienda kwake wakamhakikishia kwamba ningebadili tabia. Nilikuwa naulizwa maswali mengi na ilibidi nijibu" Alieleza Pitson.

Alisema kuwa wanawake wote ambao alikuwa anatunza walikuwa wameokoka.

"Mke wangu alirejea nyumbani ila nilikuwa nimemakinika katika kujificha. Akagundua tena na akaenda. Ilibidi wazazi wangu warudi tena kuona wazazi wake" Alisema huku akidai kuwa walikuwa wameafikiana kupeana talaka.

Hata hivyo mwanamuziki huyo alieleza kuwa walisameheana na kuahidiana kuwa mambo yale hayangejirudia.

Pitson alisema kuwa anajuta kutotumia pesa zile kwa mkewe.

(Utafsiri: Samuel Maina)