"Niko tayari kuachwa, nitaachika" Vera Sidika awasuta vikali wanaosubiri ndoa kati yake na Mauzo ivunjike ili wacheke

Vera amesema kwamba kuachwa hakumpei wasiwasi wowote kwani ako tayari kwa jambo lolote.

Muhtasari

•Mwanasoshalaiti huyo ameapa kwamba kamwe hatawahi kubembeleza mwanaume amsaidie kukimu mahitaji ya mtoto ama kumsumbua kwa kuwa anaumia moyoni.

•Vera amesema kwamba kuachwa sio jambo geni kwake kwani amewahi kutengana na watu wengi hapo awali na akaendelea na maisha yake bila tatizo.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti na mfanyibiashara mashuhuri nchini Vera Sidika amewasuta wale ambao wanasubiri atengane na mpenzi wake wa sasa Brown Mauzo ili wamcheke.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amesema kuwa  hilo halimpei wasiwasi wowote na kudai kwamba ako tayari kwa jambo lolote.

Mama huyo mtarajiwa amesema kuwa hatua ya wawili waliokuwa kwenye uhusiano kutengana ni jambo la kawaida na iwapo siku moja uhusiano kati yake na mauzo utakatika atakubali na kusonga mbele na maisha yake haraka sana.

"Eti 'tunangoja bwanako akuwache ili tukucheke hapa' eti 'wanaume watakuaibisha'.. mnajua nini, ata mimi niko tayari kuachwa na wakati itatendeka nitasonga mbele na maisha yangu haraka. Kwani nia hukumu ya kifo?  Alaa!! 

Oh! eti utawachwa na mtoto blah blah blah! Kwani ni mimi wa kwanza duniani kulea mtoto nikiwa pekee yangu?Hapana! Kwa miaka sasa nimekuwa nimejitayarisha kisaikolojia, kifedha na kimawazo" Vera amesema kwenye mtandao wa Instagram.

Mwanasoshalaiti huyo ameapa kwamba kamwe hatawahi kubembeleza mwanaume amsaidie kukimu mahitaji ya mtoto ama kumsumbua kwa kuwa anaumia moyoni.

"Nilipata ujauzito kwa masharti na wakati wangu nikiwa tayari kwa lolote. Naomba mniamboe kitu kipya sasa. Kuachwa ni jambo la kawaida..

..Kuna mabilioni ya wanaume duniani siwezi kujalishwa na mtu mmoja kuniaibisha. Kunaitwa kujipenda. Mmekataa tamaa ndio maana mnaogopa wanaume kuwaaibisha. Kama  umejipanga basi hakuna yeyote mwingine ambaye anafaa kukujalisha." Amesema Vera.

Vera amesema kwamba kuachwa sio jambo geni kwake kwani amewahi kutengana na watu wengi hapo awali na akaendelea na maisha yake bila tatizo.

Amewashauri wanawake kuwa tayari kuachwa kila wakati  na wanapoachwa wakubali na kusonga mbele na maisha yao

"Wanawake, katika maisha yako ya kuchumbiana kuwa tayari kuachwa kila wakati. Inapofanyika unawachika tu. Ni sehemu ya maisha  na tunasonga mbele kama injili. Ndio maana mimi husonga mbele haraka bila tatizo lolote na ninafurahia uhusiano wangu mpya zaidi. Yaitwa kujipenda. Niko hapa nasubiri kuaibishwa nisonge mbele kama injili, Alaaah!!" Vera amesema.