Kitumbua kimeingia mchanga ama ni kiki? Ishara zinazoashiria huenda uhusiano wa Nadia Mukami na Arrow Bwoy unayumba

Muhtasari

•Maswali mengi kuhusiana na hali ilivyo kwenye uhusiano wao yameibuka kufuatia matendo yao ya hivi karibuni kwenye mtandao wa Instagram

Image: INSTAGRAM//NADIA MUKAMI

Je, huenda wapenzi wanamuziki  Arrow Bwoy na Nadia Mukami wametengana ama ni kiki?? 

Hilo ni swali ambalo maelfu ya mashabiki wao wamekuwa wakijiuliza kufuatia matendo yao ya hivi karibuni kwenye mtandao wa Instagram.

Uvumi kuwa kitumbua kilikuwa kimeingia mchanga ulianza kuenea baada ya malkia wa muziki wa kisasa Nadia Mukami kuchapisha ujumbe wa kimafumbo  ambao uliibua hisia kuwa huenda hali sio shwari tena kati ya wawili hao.

Ujumbe wa Nadia uligusia suala la udanganyifu na ukosefu wa uaminifu kwenye uhusiano. 

"Makosa sio ajali. Kutokuwa mwaminifu na kudanganya sio makosa, ni chaguo la kujitakia. Acha kujitetea na neno 'kosa' wakati unapokamatwa" Ujumbe wa Nadia ulisoma.

Ingawa mwanamuziki huyo hakutoa maelezo zaidi kuhusiana na ujumbe wake, wengi walihisi kwamba ujumbe huo ulikuwa unaelekezwa kwa kipenzi chake.

Punde baada ya hayo ishara zaidi kuwa mambo sio mazuri pale kwenye boma la Ali Yusuf ziliibuka. 

Wapenzi hao wawili waliacha kufuatana kwenye mtandao wa Instagram, hatua ambayo sana sana huchukuliwa na watu ambao wamekosana.

Mbeleni wawili hao walikuwa wanafuatana mitandaoni ila kwa sasa ni wazi kuwa hakuna anayefuata mwingine ama huenda ata kila mmoja wao ame'block' mwenzake.

Isitoshe, Nadia amefuta picha na video zao zote ambazo alikuwa amepakia zikiwaonyesha wakiwa pamoja. 

Baada ya kufunguka kuhusu uhusiano wao mwezi uliopita wawili hao wamekuwa wakipakia video na picha si haba kwenye kurasa zao za Instagram. 

Ingawa  kwa upande wake Arrow Bwoy bado ameziweka picha zile, inaoneka mwenzake huenda hataki tena ziwe kwenye ukurasa wake.

Je, Kitumbua kimeingia mchanga ama kunani?