"Hakuna tone la pombe limewahi pita mdomo wangu" Kang'ata apuuzilia mbali madai kuwa alihutubia seneti akiwa Sabina Joy

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwandani huyo wa naibu rais amesema  kwamba kamwe hajawahi kuonja pombe maishani mwake.

•Kang'ata alipuuzilia mbali matukio yaliyo kwenye video hiyo na kusema kwamba alikuwa anatoa ombi kwa kamati ya seneti ya biashara na viwanda waeleze mbona wakulima wa Murang'a bado hawajapokea malipo ya maziwa ambayo walipeleka kwa kiwanda kinachomilikiwa na serikali ya kaunti ya Murang'a.

Seneta Irungu Kang'ata

Seneta wa Murang'a Irungu Kang'ata amepuuzilia mbali madai kwamba alihutubia kikao cha seneti akiwa anabugia vileo katika madanguro ya Sabina Joy.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, mwandani huyo wa naibu rais amesema  kwamba kamwe hajawahi kuonja pombe maishani mwake.

Kulingana na Kang'ata, sauti iliyosikika kwenye video ambayo inasambazwa mitandaoni ilikuwa ya kuongezwa na madai kuwa alikuwa kwa baa ni ya uongo.

"Wanablogu wa Kieleweke na Raila, hiyo sauti ambayo imewekwa kwa wasilisho langu kwenye seneti leo(Jumanne) kupitia njia ya mtandao ni ghushi na ya uongo.. Hakuna tone la pombe limewahi pitia mdomo wangu" Kang'ata alisema.

Kwenye video ambayo ilienezwa sana mitandaoni siku ya Jumanne, Kang'ata alisikika akikatiza spika wa seneti Ken Lusaka alipokuwa anaalika seneta wa kuteuliwa Beatrice Kwamboka na kuomba asome hotuba yake kwanza.

"Bw Spika niko hapa.. niko kwenye mtandao.. niko tayari. Bwana spika niko mtandaoni  na video yangu imewashwa" Seneta Kang'ataalisikika akisema.

Kwa kipindi spika Lusaka hangeweza  kumuona Kang'ata licha ya seneta huyo kudai kwamba video yake ilikuwa imewashwa.

"Bwana Spika video yangu imewashwa. Niko kwenye mtandao. Sijui kama ni vile nasoma ujumbe wangu ama kuna shida ya mipangilio lakini niko tayari kusoma" Kang'ata aliambia spika Lusaka.

Baada ya Kang'ata kutengeneza camera yake  maseneta waliokuwa pale seneti hatimaye waliweza kumuona na sauti zao zikaanza kupanda huku wakisikika wakijadiliana kuhusu alipokuwa seneta mwenzao.

Seneta mmoja ambaye hajatambulishwa alisikika akidai kwamba Kang'ata  alikuwa  ameketi kwa baa wala si kwa ofisi yake.

Seneta huyo alisisimua kicheko seneti alipodai kwamba Kang'ata alikuwa ametembelea chumba cha burudani maarufu jijini Nairobi cha Sabina Joy kinachojulikana kuwa madanguro .

"Bwana spika ako kwa baa! Bwana spika anakunywa busaa yake.. bwana spika ako Thika Highway anakunywa. Bwana spika ako kwa baa anakunywa... Bwana spika ako Sabina Joy" Seneta huyo alisikika akisema.

Kang'ata alijaribu kujitetea  huku akisisitiza kwamba alikuwa  ameketi kwa ofisi yake ila  kelele za burudani zingesikika huko nyuma.

"Niko kwa ofisi yangu bwana spika.. Bwana spika naomba msamaha. Naomba unipatie dakika tano nitafute mahali panapofaa"  Kang'ata alisema

Spika Lusaka alisikika akimkatiza mwandani huyo wa naibu rais kwa kuwa alikuwa amekaidi sheria za seneti na kumuarifu kwamba angempatia nafasi ya kutoa maoni yake iwapo angetafuta mahali panapofaa pa kukaa.

Baada ya uchunguzi wa kina video iliyosambazwa mitandaoni imethibitishwa kuwa ya uongo. Hii hapa video halisi ya yaliyotukia

Hata hivyo Kang'ata alipuuzilia mbali matukio yaliyo kwenye video hiyo na kusema kwamba alikuwa anatoa ombi kwa kamati ya seneti ya biashara na viwanda waeleze mbona wakulima wa Murang'a bado hawajapokea malipo ya maziwa ambayo walipeleka kwa kiwanda kinachomilikiwa na serikali ya kaunti ya Murang'a.

Kang'ata pia alitaka serikali ya kaunti ya Murang'a kueleza mbona wamiliki manyumba ambayo yanasheheni mashine za kuhifadhi maziwa pamoja na waendesha bodaboda ambazo husafirisha maziwa hawajapokea malipo yao.