"Naogopa sana uchungu wa leba" Vera Sidika aeleza kwa nini anataka kujifungua kwa njia ya upasuaji

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amekiri kwamba anahofia sana kukabiliana na uchungu wa leba.

•Mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo amesema kwamba ni heri avumilie kipindi cha uponyaji baada ya kufanyiwa upasuaji kuliko akabiliane na machungu ya leba.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti Vera Sidika amesisitiza kwamba atajifungua kwa njia ya upasuaji wala sio kwa njia ya kawaida.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amekiri kwamba anahofia sana kukabiliana na uchungu wa leba.

Mama huyo mtarajiwa amesema kwamba alifanya maamuzi kuwa angejifungua kwa njia ya upasuaji hata kabla hajapata ujauzito.

Huku ikiwa imebakia mwezi mmoja tu wakati wake wa kujifungua utimie, mwanasoshalaiti huyo ambaye anatarajia mtoto wake wa kwanza ameapa kwamba hakuna yeyote ambaye anaweza kubadilisha uamuzi wake.

"Miezi minane ya ujauzito sasa na bado nimeshikilia uamuzi wangu. Kujifungua kwa njia ya upasuaji. Niliamua haya miaka mingi kabla hata sijaamua kubeba ujauzito. Hakuna yeyote ama chochote ambacho chaweza kufanya nibadilishe uamuzi wangu. Naogopa sana uchungu wa leba Siwezi wacha kuwaza hayo licha ya kuwa nimejaribu kwa miaka mingi" Vera amesema.

Mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo amesema kwamba ni heri avumilie kipindi cha uponyaji baada ya kufanyiwa upasuaji kuliko akabiliane na machungu ya leba.

"Ndio, nimeumbwa vitofauti namna hiyo. Mimi hufanya kile nitakacho na kwa kawaida huwa tofauti na wengine wote. Chaguo langu, uamuzi wangu" Amesema Vera.

Baadhi ya wanamitandao wamekuwa wakijaribu kumshawishi mwanasoshalaiti huyo kubadili msimamo wake ila bado ameushikilia imara.

Wengi wamekuwa wakimtumia jumbe za kumuonya na kumweleza hatari zinazohusishwa na njia ya upasuaji ila Vera hajaonekana kutishika na tahadhari zile.

Hata hivyo, mwanasoshalaiti huyo amesema kwamba anatumai atajifungua mtoto mwenye afya salama.

"Wengine wanaumwa na shida zangu. Naomba nijifungue salama mtoto mwenye afya" Aliandika Vera.