Tena! Ringtone Apoko ahusika kwenye ajali nyingine ya barabarani

Muhtasari

•Apoko ambaye anafahamika sana kwa kujipiga kifua kutokana na utajiri wake alipakia picha iliyoonyesha gari lake aina ya Range Rover likiwa limegongwa na kubondeka vibaya upande wa mbele.

•Aidha Ringtone hana ustadi wa kuendesha gari ama bahati mbaya humfuata popote aendapo kwani takriban miaka miwili iliyopita alikuwa amejipata kwenye ajali nyingine.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwenyekiti wa nyimbo za injili wa kujibandika Alex Apoko maarufu kama Ringtone alihusika kwenye ajali ya barabani siku ya Jumatatu. 

Apoko ambaye anafahamika sana kwa kujipiga kifua kutokana na utajiri wake alipakia picha iliyoonyesha gari lake aina ya Range Rover likiwa limegongwa na kubondeka vibaya upande wa mbele.

Kwa kutumia kizungu kibovu mwanamuziki huyo alieleza jinsi alinusurika kifo kufuatia ajali hiyo na kumshukuru Mola kwa kumuokoa.

"Nilinusurika kutokana na ajali. Mungu ni mkuu" Apoko aliandika.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Ajali hiyo iliyotokea jana sio ya kwanza kumfanyia msanii huyo. 

Mwezi Julai mwaka huu mwanamuziki huyo asiyepungukiwa na drama alihusika kwenye ajali iliyohusisha gari mbili ndogo

Ringtone alikuwa anaendesha gari aina ya Mercedes Benz wakati aligongana na gari lingine aina ya Toyota IST.

Aidha Ringtone hana ustadi wa kuendesha gari ama bahati mbaya humfuata popote aendapo kwani takriban miaka miwili iliyopita alikuwa amejipata kwenye ajali nyingine.

Mnamo Julai 2019  gari aina ya V8 ambalo msanii huyo alikuwa anaendesha lilipoteza mwelekeo na kugonga chuma zinazowekwa kando ya barabara.