"Kwa sasa nawaruhusu kuona machozi yangu" Akothee asherehekea mabinti wake watatu kwa kumsaidia maishani

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 amesema kwamba mabinti wake wamekuwa wakimsaidia sana na kumpatia msukumo maishani.

•Vesha, Rue na Makadia walimshukuru mama yao huku wakimhakikishia jinsi wanavyompenda na kumtakia mema maishani.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri nchini Esther Akoth almaarufu kama Akothee amewasherehekea  mabinti wake watatu Vesha Okello, Rue Baby na Fancy Makadia.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 amesema kwamba mabinti wake wamekuwa wakimsaidia sana na kumpatia msukumo maishani.

Mama huyo wa watoto watano amedai kwamba Vesha, Rue na Makadia ni baadhi ya watu ambao wamechangia sana kwenye mafanikio yake makubwa na kuwashukuru sana kwa kuwepo kwao kila wakati.

"Mmekuwepo kila wakati ninapowahitaji na kunipa matumaini, angalieni mafanikio ambayo mmeweza kupata. Najua miradi yangu huwa mizito, kubwa na ya haraka. Lakini jueni kwamba nashukuru usaidizi wenu. Mungu awabariki sana,  nawashukuru sana @veshashaillan @rue.baby @fancy_makadia" Akothee alisema.

Akothee alidai kuwa ana uhakika kwamba kwa sasa mabinti wake ni wakakamavu na wanaweza kustahimili kuona akilia hadharani  anapowezwa na hisia.

"Furushi langu la furaha, siku hizi nitawaruhusu kuona machozi yangu kwa sababu najua nyinyi ni wakakamavu kabisa kuona nikilia" Alisema Akothee.

Vesha, Rue na Makadia walimshukuru mama yao huku wakimhakikishia jinsi wanavyompenda na kumtakia mema maishani.

@rue.baby Tutakuwepo nawe mama  mpendwa kila wakati

@fancy_makadia Mungu akubariki mama

@veshashaillan Tunakupenda mama

Kando na mabinti hao watatu Akothee ana watoto wengi wawili wa kiume ambao wanaishi Ulaya pamoja na 'baby daddy' wa kitinda mimba chake Prince Oyoo.