"Ameongeza kilo 6" Nana Owiti azungumzia hali ya afya ya mumewe King Kaka ambaye amekuwa akiugua miezi 4 ambayo imepita

Muhtasari

•Akiwa katika kipindi cha maswali na majibu kwenye ukurasa wa Instagram, Nana Owiti ambaye ni mke wa King Kaka alipatia mashabiki wa staa huyo hakikisho kuwa hali yake sio kama ilivyokuwa mwezi mmoja uliopita.

•Mtangazaji huyo hata hivyo alisita kufichua ugonjwa ambao mumewe amekuwa akiugua huku akisema kuwa ataufichua mwenyewe atakapokuwa tayari.

Image: INSTAGRAM// NANA OWITI

Mwanamuziki mashuhuri Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka anaendelea kupata nafuu kufuatia maradhi ambayo yamemwathiri  kwa kipindi kirefu sasa.

Takriban mwezi mmoja tu baada yake kufunguka kuhusu ugonjwa ambao ulimpata mwezi Mei na kumfanya apoteze kilo 33, hali ya afya ya rapa huyo inaonekana kuendelea kuimarika kila uchao.

Akiwa katika kipindi cha maswali na majibu kwenye ukurasa wa Instagram, Nana Owiti ambaye ni mke wa King Kaka alipatia mashabiki wa staa huyo hakikisho kuwa hali yake sio kama ilivyokuwa mwezi mmoja uliopita.

Owiti alisema kwamba wanamshukuru Mola kuona kuwa safari ya kupona ya msanii huyo inaendelea izuri na tayari amerejesha kilo 6 mwilini.

"Anaendelea vizuri kabisa. Ameongeza kilo sita na tunashuku sana kwa sababu ya hayo. Ni ushindani mkubwa . Asante kwa kuuliza" Bi Owiti alimjibu shabiki mmoja ambaye alitaka kujua kuhusu afya ya msanii huyo.

Shabiki mwingine alitaka kufahamu maradhi ambayo mume wa Bi. Owiti amekuwa akiugua.

Hata hivyo, mtangazaji huyo alisita kufichua ugonjwa ambao mumewe amekuwa akiugua huku akisema kuwa ataufichua mwenyewe atakapokuwa tayari.

"Kuhusu hilo atawaambia nyote wakati atakuwa tayari" Alisema Owiti.

Mapema mwezi uliopita Kaka alisihi mashabiki wake  kumkumbuka katika maombi yao huku akifichua kwamba hali yake ya afya ilikuwa imedhoofika kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo ilikuwa imepita.

Msanii huyo alifichua kwamba alikuwa amepoteza kilo 33 mwilini na saizi ya kiuno chake kupungua kwa inchi tatu.

Kaka alisema kuwa hata nguo alizokuwa anavaa hapo awali hazikuwa zinamtoshea tena kufuatia kupungua kwa ukubwa wa kiuno chake.