"Tunafikiria kupata mtoto wa 2,3,4" Vera Sidika apuuzilia mbali madai kuwa anajuta kupachikwa ujauzito na Brown Mauzo

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amesema kwamba walikuwa wamepangia ujauzito huo na kudai kuwa wako tayari kabisa kumkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja.

•Mwanasoshalaiti huyo amedai kwamba wanaomuonea gere wamezoea kubeba ujauzito ambao hawajapangia na ndio maana wangependa awe mwenye majuto pia.

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 31 pia amewasuta baadhi ya wanamitandao ambao walitaka sura yake iharibike kufuatia ujauzito ambao amebeba.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri nchini Vera Sidika ameweka wazi kwamba kamwe hajuti kupachikwa ujauzito na mpenzi wake Brown Mauzo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Vera amesema kwamba walikuwa wamepangia ujauzito huo na kudai kuwa wako tayari kabisa kumkaribisha mtoto wao wa kwanza pamoja.

Mama huyo mtarajiwa amepuuzilia mbali madai kuwa anajuta kubeba ujauzito huku akisema kwamba anatazamia kubeba ujauzito mwingine punde baada ya kujifungua kifungua mimba chake hivi karibuni.

"Vile tuko hapa tunafikiria kuhusu mtoto wa pili punde baada ya Mungu kutujalia binti wetu, Inshallah, na tena mtoto wa tatu na wa nne pamoja na mwanaume mmoja, mume wangu. Halafu kuna watu wanataka kusema eti najuta, LMAOOO. Huwa sifanyi makosa. Huwa napanga maisha yangu yote" Vera alisema

Mwanasoshalaiti huyo amedai kwamba wanaomuonea gere wamezoea kubeba ujauzito ambao hawajapangia na ndio maana wangependa awe mwenye majuto pia.

Vera amesisitiza kuwa ako tayari kujenga familia imara pamoja na mwanazmuiki Brown Mauzo ambaye wamekuwa wakichumbiana naye kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

"Nadhani baadhi yenu wenye chuki mmezoea kubeba ujauzito ambao hamjapangia hata hamuwezi amini kuwa mtu anaweza kuwa tayari na kupanga familia kutoka mwanzo. Kwa kuwa hamuamini sasa mnataka wanawake wengine wajawazito wawe na majuto. Endelea kutaka. Tumekuwa tayari, wenye furaha na kung'aa hadi mwisho" Alisema Vera.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 31 pia amewasuta baadhi ya wanamitandao ambao walitaka sura yake iharibike kufuatia ujauzito ambao amebeba.

"Watu walidhani eti  Vera Sidika akiwa mjamzito atachapa kama wao. Hawaamini kuwa hata nakaa vizuri zaidi nikiwa mjamzito kuliko siku za kawaida" Vera alidai.