Sauti Sol watengana kwa muda, Kila mmoja kufanya muziki kivyake

Muhtasari

•Kikundi hicho  ambacho kimepokea tuzo nyingi kutokana na ubora wa muziki wao kimesema kuwa kila mmoja wao atafanya kazi pekee yake hadi mwezi Mei mwaka ujao.

•Kila mmoja wao anatazamia kuwa wametoa ngoma kivyake kufikia mwezi Desemba mwakani huku Bien akizindua mradi huo kwa kutoa kibao 'Bald Men Anthem' ambacho ameshirikisha  Aaron Rimbui.

Image: INSTAGRAM

Kikundi cha muziki mashuhuri nchini Sauti Sol kimetangaza utengano wa muda kati ya wanabendi wake Bien, Savara, Chimano na Polycarp Otieno.

Kupitia kwa barua ya wazi kwa mashabiki, kikundi hicho  ambacho kimepokea tuzo nyingi kutokana na ubora wa muziki wao kimesema kuwa kila mmoja wao atafanya kazi pekee yake hadi mwezi Mei mwaka ujao.

Wanne hao ambao kwa sasa wako katika ziara ya muziki nchini Marekani wamepatia mradi huo jina 'Alone Together' (Pekee Pamoja) na kudai kuwa wazo hilo lilifuatia tafakari ya kina ya wanabendi wakati wa janga la Corona.

Kila mmoja wao anatazamia kuwa wametoa ngoma kivyake kufikia mwezi Desemba mwakani huku Bien akizindua mradi huo kwa kutoa kibao 'Bald Men Anthem' ambacho ameshirikisha  Aaron Rimbui.

"Kwa kila ngoma mashabiki wetu wa kitambo na wapya, wazee na wadogi mtaweza kuona na kusikia talanta zetu na mfahamu mengi zaidi kuhusu mbona sisi ni viungo vinne muhimu ambavyo vinatengeza bendi moja" Sauti Sol walisema.

Hata hivyo wametangaza kuwa wataendeleza biashara zao mbalimbali pamoja kama vile Sauti Sol Entertainment. Sauti Sol Records, Pacesol.

"Pia tunajivunia mafanikio ya Bensoul na Nviri The Storyteller kupitia usaidizi wa timu yenye talanta inayowazingira" Walimaliza kwa kusema.