Mchekeshaji Eric Omondi amlipa Butita milioni 3.5 ili amwandikie na aelekeze shoo ya 'Wife Material 3'

Muhtasari

•Eric anapanga kuzindua shoo ya Wife Material 3 mnamo siku ya Jumanne wiki ijayo, miezi minne tu baada ya onyesho la pili la shoo hiyo kuvurugika.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Mchekeshaji maarufu nchini Eric Omondi amekamilisha malipo ya shilingi milioni 3.5 kwa msanii mwenzake Eddie Butita kama ada ya kuandikiwa shoo yake ya Wife Material 3.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Omondi kufichua kuwa Butita alimdai kitita kikubwa kisichopungukia dola 35,000.za Marekani ndiposa akubali kumwandikia na kuelekeza shoo yake.

Hapo awali, Butita ambaye hivi majuzi alifanya kazi na kampuni mashuhuri ya kutengeneza filamu  ya Netflix alikuwa ameagiza Omondi kulipa ada hiyo kabla hajaanza kazi ile.

"@ericomondi kama nilivyokwambia mapema, timu yangu imesisitiza kulipisha ada ya dola 35,000 za Marekani kabla ya kazi juu wewe ni mtu wetu. Ambia wasimamizi wako wafanye hivo" Butita alimwandikia Omondi kupiitia mtandao wa Instagram.

Omondi alisema kuwa ako tayari kulipa ada hiyo ila alialamika kuwa Butita alikuwa hashiki simu zake ili wapate kujadiliana zaidi.

Alimsihi Butita akubali wawasiliane kwa simu moja kwa moja badala ya kumtuma kwa wasimamizi wake

Hii nidio tatizo na sekta yetu ya burudani @ddiebutita sio tu rafiki yangu mzuri sana bali pia ninamuona kama ndugu yangu. Lakini Sasa akianza Kusema eti  napaswa kuzungumza na timu yake na hachukui simu zangu..

Kwa nini unitume kwa meneja wako ilhali twaweza kuzungumza na kufanya biashara??.Sisi Hatuna shida ya  pesa, tunakuita tu kutoa huduma zako za kitaaluma. Ama juu  ya Netflix sasa umeingiwa na kiburi?! Shika simu zangu shoo itaanza wiki ijayo Jumanne na tunakuhitaji. Umedai dola 35,000 ambazo ni takriban milioni 3.5 na tuko tayari kulipa hata zaidi @eddiebutita" Eric alimwambia Butita kupitia mtandao wa Instagram.

Siku ya Jumatano Eric alipakia video iliyoonyesha akimkabidhi Butita hundi nne za benki kuthibitisha kuwa alikuwa amekamilisha kumlipa ada yake.

Hundi tatu zilikuwa za shilingi laki tisa huku ingine moja ikiwa ya shilingi laki nane.

"Imekamilika!! Shilingi 3,5. Wacha mchezo uanze sasa!! Tarehe 19 Oktoba!! @eddiebutita" Eric aliandika chini ya Video hiyo.

Eric anapanga kuzindua shoo ya Wife Material 3 mnamo siku ya Jumanne wiki ijayo, miezi minne tu baada ya onyesho la pili la shoo hiyo kuvurugika.