'Nirudishie pesa zangu!' Ringtone aghadhabishwa na wimbo wa Mr. Seed 'Dawa ya baridi', adai kuwa sio wa injili

Muhtasari

•Kulingana na Ringtone, dawa ya baridi pekee ni maji moto yaliyotiwa ndimu pamoja na kuota jiko la makaa wala sio mwanamke yeyote.

•Apoko alisema kwamba sekta ya Injili nchini imefifia na kudai kuwa wanamuziki pekee waliobaki kwenye injili ni yeye, Daddy Owen , Guardian Angel pamoja na wengine wachache.

Ringtone Apoko, Mr Seed
Ringtone Apoko, Mr Seed
Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko ameonekana kutoridhishwa na albamu mpya ya msanii mwezake Mr Seed 'Black Child' ambayo ilizinduliwa mwezi uliopita.

Apoko ambaye anatambulika sana kutokana na drama chungu nzima ambazo zimezingira maisha yake amedai kuwa Seed alidanganya wasanii wengine wamchangie pesa aweze kuzindua albamu ya Injili ilhali alitaka kuzindua albamu ya nyimbo za kidunia.

Amekosoa vikali albamu ya Seed haswa wimbo 'Only One' (Dawa ya Baridi) ambao ameshirikisha Masauti.

Kulingana na Ringtone, dawa ya baridi pekee ni maji moto yaliyotiwa ndimu pamoja na kuota jiko la makaa wala sio mwanamke yeyote.

"Alitudanganya tukaenda kwa hafla yake kumchangia tukidhani eti ni nyimbo za Mungu kumbe alikuwa anatoa wimbo akisema wanawake ndio dawa ya baridi. Mwanamke hawezi kuwa dawa ya baridi. Dawa ya baridi ni ukunywe maji moto ya ndimu ama uchukue makaa uweke kwa jiko oute" Ringtone alisema.

Apoko alimsihi Seed amrejeshee shilingi elfu hamsini ambazo zilikuwa mchango wake wakati wa uzinduzi wa albamu 'Black Child' takriban mwezi mmoja uliopita.

"Mr Seed ni conman. Kwa kweli ningependa anirudishie pesa zangu ambazo nilimpatia. Mi nilimpatia takriban 50,000.. Mr Seed tulimpea pesa akitudanganya anazindua albamu ya Injili, kumbe alikuwa anazindua nyimbo za kidunia" Alisema Apoko.

Msanii huyo mzaliwa wa Kisii alikuwa anahutubia wanahabari katika hafla ya kuzindua albamu ya Daddy Owen ambayo ilifanyika siku ya Jumamosi.

Apoko alisema kwamba sekta ya Injili nchini imefifia na kudai kuwa wanamuziki pekee waliobaki kwenye injili ni yeye, Daddy Owen , Guardian Angel pamoja na wengine wachache.