'Paul na Eddie walikuwa wanajaribu kutenganisha vita kati ya wanawake wawili,' Wapi Pay yatetea mume wa Janet Mbugua na pacha wake

Muhtasari

•Wapi Pay imesema kwamba kuna hali ya kutoelewana kuhusiana na video hiyo ikidai kwamba wawili hao walikuwa wanajaribu kutenganisha vita kati ya wanadada hao wawili wala sio eti walikuwa wanawashambulia kama wengi wanavyoamini.

•.Wapi Pay imeomba watu wasite kueneza habari potofu bila msingi wa ukweli kuhusiana na yaliyojiri usiku huo.

Mapacha Paul Ndichu na Eddie Ndichu
Mapacha Paul Ndichu na Eddie Ndichu
Image: INSTAGRAM// WAPI PAY

Kampuni ya Wapi Pay imejitokeza kutetea waanzilishi wenza Eddie na Paul Ndichu ambao walihusika kwenye mvurugano na wanawake wawili  siku ya Jumamosi.

Video ambayo imeenezwa sana mitandaoni inaonyesha mapacha hao wawili wakiwa katika hali ya mvutano na wanadada  wawili katika hoteli ya Ole Sereni jijini Nairobi. Haijabainika wazi kilichokuwa kimesababisha mzozo yule.

Hata hivyo Wapi Pay imesema kwamba kuna hali ya kutoelewana kuhusiana na video hiyo ikidai kwamba wawili hao walikuwa wanajaribu kutenganisha vita kati ya wanadada hao wawili wala sio eti walikuwa wanawashambulia kama wengi wanavyoamini.

Kupitia ujumbe ambao ulitolewa kwa wanahabari asubuhi ya Jumanne, Wapi Pay imeomba watu wasite kueneza habari potofu bila msingi wa ukweli kuhusiana na yaliyojiri usiku huo.

"Tunafahamu kuhussu video ambayo inaenezwa mitandaoni kuhusiana na mvurutano uliohusisha Eddie na Paul Ndichu, waanzilishi wenza wa kampuni, katika hoteli moja Nairobi usiku wa Jumamosi.

Tullipata habari hizo bila ladha na zikiwa za kusumbua na tungependa kusema kuwa tabia yoyote inayohusisha ukatili dhidi ya wanawake haziashirii maadili yetu wala ya Eddie na Paul. Tunavyoelewa ni kwamba video hiyo ambayo ni yakutisha  haionyeshi matukio ya kweli ambayo yalitokea usiku huo. Kusema kweli, Paul na Eddie walihusika katika jaribio la kudhibiti vita kati ya wanawake wawili na kujilinda kutokana na wachokozi fulani. 

Kesi hiyo imeripotiwa kwa polisi na DCI kwa uchunguzi zaidi na suluhu. Tunaposubiria haya, tunawaomba mjizuie kusambaza habari potofu ambazo hazina msingi wa ukweli" Ujumbe wa Wapi Pay ulisoma.

Kampuni hiyo imesema kwamba inamejengwa kwa tamaduni ya kuheshimu waajiriwa wote , wateja  na haikubali ubaguzi wa aina yoyote wala matendo ya ukatili wa kijinsia.