Boniface Mwangi asema nyumba yake imebomolewa amshutumu mwanasiasa mashuhuri

Muhtasari

•Kando na nyumba kulipuliwa, mwanaharakati huyo pia  amedai kwamba majambazi wale walishambulia wafanyikazi wake na kuwaibia vitu mbalimbali.

•Mwangi amehusisha mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini na tukio hilo huku akitoa ombi kwa serikali kulichunguza  kwa kina .

Image: INSTAGRAM// BONIFACE MWANGI

Mwanaharakati mashuhuri nchini Boniface Mwangi amejitokeza kulalamika baada yake iliyo katika eneo la Lukenya kaunti ya Machakos kulipuliwa na magaidi wasiojulikana usiku wa Jumatano.

Kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mwangi alipakia video inayoonyesha msingi wa  nyumba ambayo inaendelea kujengwa ukiwa umelipuliwa.

Kando na nyumba kutupiwa bomu, mwanaharakati huyo pia  amedai kwamba majambazi wale walishambulia wafanyikazi wake na kuwaibia vitu tofauti.

"Majambazi walivamia nyumba yangu ambayo inajengwa, wakalipua msingi wa nyumba na kuibia wafanyikazi wangu. Siwezi enda huki kwa sababu za kiusalama" Mwangi alisema.

Baba huyo wa watoto watatu amesema kwamba risasi ambazo zilitumika pamoia na vilipuzi vingali katika eneo la tukio.

Mwangi amehusisha mwanasiasa mmoja mashuhuri nchini na tukio hilo huku akitoa ombi kwa serikali kulichunguza  kwa kina .

"Risasi na vilipuzi vingali katika eneo la tukio. Kwani tunaishi katika nchi gani?.. Bado siogopi kwani Mungu ni mchungaji wangu, sitataka zaidi, atanilinda.. Kwa serikali, risasi na vilipuzi vingali kwa kiwanja changu. Ninachoomba ni muanzishe uchunguzi wa kina na wazi. Kama kuongea ukweli kutafanya niuliwe, niko tayari kufa. Naumia lakini roho yangu bado haijavunjika. Hata haya yatapita" Mwangi alisema.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanaharakati huyo kushambuliwa sana mitandaoni kutokana na kujihusika kwake sana kwenye mahusiano kati ya Lilian Ng'anga na mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani.