"Nilitazama, nikasikia kila kitu!" Vera Sidika asimulia aliyopitia alipokuwa anajifungua kwa njia ya upasuaji

Muhtasari

•Vera amesema kwamba alichagua kujifungua tarehe 20 Oktoba ili bintiye awe anasherehekea siku ya kuzaliwa pamoja na wao nyumbani kwani ni siku ya likizo ya umma.

•Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 31  alijifungua kwa njia ya upasuaji almarufu kama CS kama  ilivyokuwa mapenzi yake.

•Vera ameeleza kwamba alikuwa ameamka wakati upasuaji ulikuwa unaendelea na alishuhudia kila kitu ambacho madaktari wake walimfanyia.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Tarehe 20 mwezi Oktoba itabaki kuwa siku muhimu sana maishani mwa mwanasoshalaiti Vera Sidika na mpenzi wake Brown Mauzo.

Kando na maadhimisho ya siku ya mashujaa, hiyo ndiyo tarehe ambayo wanandoa hao walikaribisha binti ya Asia Brown Duniani. 

Vera alitangaza kwamba alijifungua mtoto wake wa kwanza mida ya saa nne na dakika 21 asubuhi ya Jumatano.

"Tarehe 20.10.2021 mida ya saa nne na dakika 21 asubuhi, mtoto wa malkia alizaliwa. Asia Brown @princess_asiabrown. Utaishi kuwa miujiza ambayo itafanya maisha yetu yawe kamili" Vera alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Vera amesema kwamba alichagua kujifungua tarehe 20 Oktoba ili bintiye awe anasherehekea siku ya kuzaliwa pamoja na wao nyumbani kwani ni siku ya likizo ya umma.

Mwanasoshalaiti huyo mwenye umri wa miaka 31  alijifungua kwa njia ya upasuaji almarufu kama CS kama  ilivyokuwa mapenzi yake.

Alisema kwamba alijifungua salama kabisa  na kuhakikishia mashabiki wake kwamba bintiye ako mzima pia.

"Natamani nyote mngeweza kumuona msichana wetu mdogo. Mungu wangu!! Ako mzima na ni mrembo. Mama yangu amekuwa akiangalia picha zake tangu alipotoka tumboni. Tayari anapanga kuenda naye Mombasa. Wah!! Naona wivu kila anapolala. Nataka tu aamke ili nione macho yake mazuri. Mungu ni mwema" Vera alisema.

Mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo amesimulia kwamba mchakato wa kujifungua kwa njia ya upasuaji uliendelea vyema bila tatizo lolote.

Vera ameeleza kwamba alikuwa ameamka wakati upasuaji ulikuwa unaendelea na alishuhudia kila kitu ambacho madaktari wake walimfanyia.

Hata hivyo amesema kwamba hakuhisi uchungu wowote kwani  alikuwa amepewa dawa za kuzuia uchungu na kufichua kuwa hajashuhudia machungu yoyote hata baada ya upasuaji.

"Imekuwa masaa 21 baada ya upasuaji. Bado sihisi uchungu wowote. Naweza kuamka, kutembea pekee yangu, wah!! Hata mimi nimeshangaa. Kusema kweli niliskia vizuri wakati wa upasuaji. Niljihisi kama napaa. Nilikuwa nimeamka, niliona na nikaskia kila kitu. Hata nilisimulia daktari wangu hadithi huku nyimbo aina za RNB zikicheza" Vera aeleza.

Vera amesema kwamba uamuzi wake wa kujifungua kwa njia ya upasuaji ndio uamuzi bora amewahi kufanya maishani.