"Mimi ni mtu wa bangi!" Mwigizaji Robert Agengo afichua alianza kuvuta bangi katika shule ya msingi

Muhtasari

•Agengo alisema kwamba alitumia bangi kwa mara ya kwanza takriban miaka ishirini na minane iliyopita.

•Alifichua kwamba alipokuwa katika darasa la nane aliwahi kunywa chai iliyochanganywa na bangi ambayo alipikiwa na mpenzi wake

Image: INSTAGRAM// ROBERT AGENGO

Mwigizaji mashuhuri Robert Agengo amekiri kwamba yeye ni mtumizi wa mihadarati aina ya bangi.

Akiwa kwa mahojiano na Buzz Central Kenya hivi karibuni, mwigizaji huyo alifichua kwamba alianza kuvuta bangi akiwa katika shule ya msingi.

Agengo ambaye anafahamika sana kutokana na kipindi cha Zora ambapo ni mmoja wa waigizaji wakuu alisema kwamba alitumia bangi kwa mara ya kwanza takriban miaka ishirini na minane iliyopita.

"Mimi ni mtu wa bangi. Nilianza kuvuta bangi mwaka wa 1998. Hiyo ilikuwa kabla ya kujiunga na shule ya upili. Najua watu wazee zaidi ambao wanavuta" Agengo alisema.

Alifichua kwamba alipokuwa katika darasa la nane aliwahi kunywa chai iliyochanganywa na bangi ambayo alipikiwa na mpenzi wake.

"Mimi nishawahi kunywa bangi nikiwa katika darasa la nane. Unachemshiwa unakunywa. Nilikuwa na mpenzi ambaye alinipikia chai ya bangi nikakunywa" Alifichua Agengo.

Agengo alidai kwamba hajawahi patwa na athari zoyote mbaya kutokana na uvutaji bangi huku akieleza kuwa wale ambao huathirika ni kwa sababu ya kuzichanganya na dawa zingine. 

Kando na utumizi wa bangi, msanii huyo alikiri kwamba aliwahi kufanya maovu zaidi ambayo alisita kufichua.