Mke wa Babu Owino afunguka kuhusu mahusiano yao na kueleza kwa nini huwa anamvumilia mumewe licha ya yote

Muhtasari

•Bi Muthoni alitoa sababu za kumvumilia mwanasiasa huyo licha ya maovu yote ambayo amehusishwa nayo katika taaluma yake ya siasa huku akimtaja kama mtu mwema.

•Mfanyibiashara huyo tajika alisema kwamba huwa anazielewa tabia za Owino kwa kuwa anafahamu fika alilelewa katika mtaa wa mabanda.

•Babu Owino alisema kuwa alifahamu kwamba Fridah ndiye chaguo la moyo wake punde tu alipomuona kwa mara ya kwanza.

Image: INSTAGRAM// BABU OWINO

Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu  kama Babu Owino pamoja na mke wake Fridah Muthoni wamefunguka kuhusu mahusiano yao na kinachowaweka pamoja licha ya yote.

Hivi karibuni wawili hao ambao wamekuwa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka kumi na miwili  walishiriki katika mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali maishani mwao.

Bi Muthoni alitoa sababu za kumvumilia mwanasiasa huyo licha ya maovu yote ambayo amehusishwa nayo katika taaluma yake ya siasa huku akimtaja kama mtu mwema.

" Wewe ni mtu mwema. Hilo ndilo neno linalokuzungumzia wewe. Uko na moyo wa dhahabu. Niliweza kuona hayo, labda kwa usaidizi wa roho mtakatifu. Tangu siku ya kwanza nilipokuona nilijua kuwa wewe ni mtu mwema. Ulikuwa unaniambia eti wewe ni kama nazi. Mgumu nje lakini laini ndani. Ulikuwa mpole kwangu na niliweza kuona uzuri wako" Muthoni alisema.

Mfanyibiashara huyo tajika alisema kwamba huwa anazielewa tabia za Owino kwa kuwa anafahamu fika alilelewa katika mtaa wa mabanda.

"Sio wengi ambao huwezi kutoka mtaa wa mabanda. Ni rahisi kuchukua mambo ambayo yataathiri tabia zako kidogo. Yanaweza kosa kubadilisha moyo wako lakini nje waweza onekana kuwa mtu tofauti. Yale ambayo watu huona na kusema juu yako huwa najua si ya kweli kukuhusu. Wewe ni mtu mwema. Huwa unagusa maisha ya watu wengi.. wewe ni mtu jasiri. Huwa unaanguka kisha unajiinua tena" Alieleza Muthoni.

Muthoni pia alisema kuwa mara kwa mara huwa anapatana na watu ambao hutoa ushahidi kuhusu wema na ukarimu wa mumewe.

Kwa upande wake Babu Owino alisema kuwa alifahamu kwamba Fridah ndiye chaguo la moyo wake punde tu alipomuona kwa mara ya kwanza.

Alimshukuru Maulana kwa kumjalia mke anayemsaidia kusuluhisha matatizo yake wala sio anayemletea matatizo.

"Nashukuru Mungu nilioa suluhu sio tatizo" Babu alisema.