"Singeweza kutembea" King Kaka afunguka kuhusu wakati ugonjwa ulimzidia hadi akakubali kulazwa hospitalini

Alifichua kwamba alikubali kulazwa hospitalini wakati ugonjwa ulikithiri na akaishiwa na nguvu mwilini.

Muhtasari

•Kwa kipindi cha siku tatu kabla ya kulazwa hospitali mwanamuziki huyo alikuwa anatapika sana na kuendesha kila wakati.

•Baada ya kuona kuwa kweli alikuwa amelemewa, baba huyo wa watoto watatu alikubali kuenda kulazwa katika hospitali.

•Kaka alisema kufikia wakati alikuwa anaenda kulazwa hospitalini alikuwa ameishiwa na nguvu kabisa na alikuwa ameshindwa hadi kutembea.

Nana Owiti na King Kaka
Nana Owiti na King Kaka
Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amefunguka kuhusu wakati alizidiwa na ugonjwa hadi akalazwa hospitalini.

Akiwa kwenye mahojiano na mke wake Nana Owiti hivi karibuni, rapa huyo alifichua kwamba alikubali kulazwa hospitalini wakati ugonjwa ulikithiri na akaishiwa na nguvu mwilini.

Kwa kipindi cha siku tatu kabla ya kulazwa hospitali mwanamuziki huyo alikuwa anatapika sana na kuendesha kila wakati.

"Nilianza kutapika na kuendesha kwa siku tatu mfululizo. Hata nilishindwa kutembea. Kuna siku niliamka nilikuwa nahitaji kuenda kutapika, nilienda kama nimeshikilia ukuta. Niliishiwa na nguvu kabisa. Sijui kama nilipoteza kilo tano nilipoteza hizo siku tatu. Mpaka nikatumana ndoo ili niweze kuitapikia nikiwa hapo tu kwa kitanda" King Kaka alisimulia.

Mwanzoni alipelekwa hospitalini na akatibiwa maumivu yakatulia kidogo kisha akaruhusiwa kwenda nyumbani.

Usiku huo hata hivyo hakuweza kupata hata lepe la usingizi kwani alishinda akijipindua kwa kitanda kwa kuwa hakuwa na starehe hata kidogo.

Baada ya kuona kuwa kweli alikuwa amelemewa, baba huyo wa watoto watatu alikubali kuenda kulazwa katika hospitali.

"Mimi singewahi kubali niende hospitalini. Lakini asubuhi iliyofuata nikaambia Nana tuende. Jinsi nilikuwa nahisi, kila kitu kilikuwa kimeharibika. Tulienda kuangaliwa katika hospitali ya Nairobi. Niliambia Nana tukishatoka kuangaliwa anipeleke kwa hospitali yoyote ambayo tutapata nitalala huko" Kaka alisema.

Bi Owiti alisema alikuwa anaona mumewe amelemewa ila hakutaka kumwambia mwenyewe akalazwe hospitalini. Alitaka King Kaka mwenyewe akubali kuenda. 

Kaka alisema kufikia wakati alikuwa anaenda kulazwa hospitalini alikuwa ameishiwa na nguvu kabisa na alikuwa ameshindwa hadi kutembea.

"Hiyo siku nilishindwa kutembea. Ilikuwa lazima nishikilie mtu nitumie nguvu yangu ya mwisho kutembea. Tulienda katika hospitali ya Nairobi nikaambiwa eti labda nilikuwa naugua COVID kwa kipindi kirefu na dalili nilizokuwa nazo ni zenye zilikuwa zimebaki. Waliangalia kama nilikuwa na homa ya matumbo. Tulisema tuende kwa ile hospitali tulikuwa tumechagua nilazwe hapo South C. Tulipoingia niliwekwa kwa kiti cha magurudumu. Waliniuliza kama walete kiti hicho ama ningeweza kutembea nikawaambia walete" King Kaka alisema.

Alipokuwa pale hospitalini alifanyiwa vipimo kadhaa na ikabainika hakuwa anaugua ugonjwa wa COVID .

Baada ya kufanyiwa vipimo na kupata matokeo mwanamuziki huyo alipelekwa katika wadi ambapo alilazwa.

King Kaka alisema alipolazwa aliwekwa mipira ambayo ingesaidia kupeleka chakula mwilini kwani hakuwa anaweza kula.

"Hizo siku tano kabla niende hospitali sikuwa nakula. Nilikuwa nakonda, nilikuwa natapika. Kuingia hospitalini nikawekwa mipira.Hizo siku tatu za kwanza bado nilikuwa napatiwa chakula kwa mipira. Nadhani huo ndio ulikuwa wakati mgumu zaidi. Nilianza kutapika damu. Usiku wa pili mwili wangu ulikuwa na joto sana" Alisema.

Baada ya kulala hospitalini siku tatu mwanamuziki huyo alianza kupata ndoto za kuogofya ambazo hazikuwa zinaisha.

"Nilijiuliza nimechizi ama? Nikaanza kujiona Kencom nafoka nikiwa nimechizi alafu watu wananipatia chakula. Niliona nikiwa nimechizi. Ilikuwa saa tisa usiku nikaamka nikasema labda wauguzi wangenieleza. Nikauliza miuuguzi kama nimechizi na hawaniambii. Aliniambia labda ni joto ilikuwa imenizidia kwa mwili" Alisema.

Kwa kuwa hakuwa anaweza kula alianza kupatiwa mafunzo kuhusu jinsi angeweza kula ila haikuwa rahisi kwake.

"Nilikuwa nachukua kijiko nauma chakula natafuna kwa dakika 30. Nilikuwa nahisi kutapika. Nilikuwa nasoma kula" Alisema

Alisema alipata motisha wa kujikaza kula baada ya kufikiria kuhusu familia yake na jinsi alivyotaka sana kuona watoto wake tena.

King Kaka alisema hatua yake kupona ugonjwa huo ilifanya mapenzi yake kwa Mungu yakawa makubwa zaidi hukua akieleza kuwa maombi yalimsaidia sana kupona.