"Mtoke hapa Nairobi mrudi ushago!" Eric Omondi awashambulia wachekeshaji wenzake

Muhtasari

•Kulingana na Omondi, wacheshi wa Kenya hawaonyeshi juhudi zozote za kuboresha sekta ya ucheshi nchini na wanachosha sana.

•Mchekeshaji huyo amesema Kenya inahitaji kizazi kipya cha wachekeshaji ili kuokoa sekta hiyo kabla izame kabisa.

Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Baada ya kuwashambulia wanamuziki wa Kenya kwa kipindi cha takriban siku kumi zilizopita  akidai kuwa wamelala, Eric Omondi sasa amewageukia wachekeshaji wenzake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama amedai wasanii wa Kenya wamekosa mwelekeo, ubunifu pamoja na maono.

Kulingana na Omondi, wachekeshaji wa Kenya hawaonyeshi juhudi zozote za kuboresha sekta ya ucheshi nchini na wanachosha sana.

"Kama kuna kikundi cha watu ambacho kimekosa mwelekeo, ubunifu na maono ni wacheshi. Hakuna bidii!!! Ni kundi linalochosha zaidi la watumbuizaji nchini!!" Omondi amesema.

Omondi amedai wachekeshaji wa Kenya wana mazoea ya kurudia vichekesho vya hapa nchini tu mara kwa mara, jambo ambalo limewafanya wakose kupata nafasi za kutumbuiza nje ya mipaka ya Kenya.

 Amejipiga kifua kuwa yeye pekee ndiye aliyeshikilia sekta ya uchekeshaji kutokana na ubunifu  na majukumu makubwa anayofanyia jamii huku akilalamika kuwa sasa amechoka.

Katika nchi yenye Watu milioni 46 hakuna mchekeshaji hata Mmoja ame kwenda nje ya mipaka. Kila kitu kuanzia vichekesho vyao hadi uzalishaji ni ya hapa tu!! Kufanya kitu kimoja miaka nenda miaka rudi!! Nimechoka!!! Kila Kitu ni Eric Omondi!!! Kujaza nyanja Kenya na Tanzania Eric Omondi!!! Shoo za kimataifa, Eric Omondi!! Ridhiki Eric Omondi!! Ubunifu, Eric Omondi!!! Kushughulikia masuala ya jamii Eric Omondi!!! Kila kitu itakua ni Eric Tu??? Nimechoka!! Ikiwa huwezi kuinua bendera basi usijiite mchekeshaji na mtoke hapa jijini muende ushago!!!Mtu mmoja anawezaje kubeba sekta moja.Nimechoka, Punda amechoka!" Omondi amesema.

Mchekeshaji huyo amesema Kenya inahitaji kizazi kipya cha wachekeshaji ili kuokoa sekta hiyo kabla izame kabisa.